Waziri wa Maji, Nishati, Ardhi na Mazingira, Salama Aboud Talib
alisema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuanza
kwa kazi za utafiti wa nishati ya mafuta na gesi kwa kutumia ndege,
itakayoruka hewani na kupiga picha mbali mbali katika maeneo ya ardhi.
Alisema suala la mazingira limepewa kipaumbele cha kwanza katika kazi
za mafuta, na sehemu ambayo nishati hiyo itagundulika, maslahi ya
wananchi yatazingatiwa kwa kiwango kikubwa.
Alifafanua kuwa, maslahi yao yatalindwa ikiwemo kulipwa fidia baada
ya kuhamishwa na kupisha kazi za uchimbaji wa mafuta na gesi.
“Kazi za utafutaji wa mafuta na gesi zimeanza rasmi na
tunawahakikishia wananchi kwamba maslahi yao yatalindwa kwa sababu
tutazingatia uhifadhi wa mazingira katika zoezi hilo,” alisema.
Alisema makubaliano na kampuni itakayofanya kazi za utafiti
yamezingatia maslahi mapana ya wananchi, hivyo hakuna matatizo
yanayoweza kujitokeza wakati kazi za utafutaji mafuta zikifanyika
nchini.
Aidha, alisema Serikali bado inaendelea na utafiti wa kazi ya
utafutaji nishati mbadala ikiwemo umeme wa jua na mawimbi ya bahari ili
kuifanya Zanzibar kuwa na nishati ya uhakika.
Alisema tafiti hizo zinaendelea kufanywa kwa kushirikiana na ufadhili
wa jumuiya ya Ulaya (EU) kwa kujenga vituo vya majaribio vya utafiti wa
nishati ya jua na mawimbi ya bahari.
“Tunaendelea na kazi za utafiti wa nishati mbadala ambao utatuwezesha
kuwa na vyanzo vyetu vya kuzalisha umeme kwa ajili ya
maendeleo’alisema.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Maji, Nishati na
Mazingira Ali Halik Mirza, alisema juhudi zinaendelea za kuhakikisha
Zanzibar inapata nishati ya umeme mbadala itakayopunguza matumizi na
kutegemea umeme kutoka Tanzania Bara kupitia Shirika la Umeme Tanzania
(Tanesco).
“Kazi ya kutafuta nishati mbadala ya nguvu za umeme ni endelevu na
muhimu kwa Zanzibar ili kuwa na umeme wake ambao unaweza kutumika wakati
wa dharura,” alisema.
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeanza kazi ya utafutaji nishati
ya mafuta na gesi kufuatia Baraza la Wawakilishi kupitisha mswada wa
mafuta na gesi na kutiwa saini na rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed
Shein.
Kampuni ya Bell Geospace kutoka Uingereza imepewa kazi ya kutafuta
nishati ya mafuta na gesi kwa niaba ya kampuni ya Ras Gas kutka
RasKhaimah.
chanzo:Habarileo.
Comments