Wanafunzi wamuunga mkono JPM vita dawa za kulevya..

Rais John MagufuliWAHITIMU wa kidato cha sita katika Shule ya Sekondari ya St Mathew’s iliyopo Mkuranga mkoani Pwani, wamempongeza Rais John Magufuli kwa kupambana na tatizo la matumizi ya dawa za kulevya hali itakayowaokoa vijana wengi wanaoangamia kutokana na dawa hizo.
Katika risala yao iliyosomwa na Saudi Zaidi mwishoni mwa wiki, wanafunzi hao walisema:
“Tunapongeza juhudi zinazofanywa na Rais Magufuli katika kupambana na matumizi ya dawa za kulevya, kwani vijana wengi wanaotumia dawa hivi sasa wamepoteza dira na hali hiyo inachangia hata taifa kupoteza nguvu kazi.”
Aidha, wanafunzi hao waliiomba serikali iweke utaratibu wa kutobadilisha mitaala mara kwa mara, kwani hali hiyo huwafanya washindwe kujua kitu gani wakisome ili kiwawezeshe kufanya vizuri katika mitihani yao ya mwisho.
Akizungumza katika mahafali hayo ya 12, Mkuu wa shule hiyo, Christopher Segereti alisema zaidi ya wanafunzi 400 wanatarajiwa kufanya mitihani ya kidato cha sita.
Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga aliyekuwa mgeni rasmi katika mahafali hayo, Filbeto Sanga alimpongeza mmiliki wa shule hiyo, Thadeo Mutembei kwa kuwa na shule nne katika wilaya yake ambazo zimekuwa msaada mkubwa.
chanzo:Habarileo.

Comments