Waagiza matumizi Kituo Mahiri cha Kutunzia Kumbukumbu.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Profesa Norman SigalaKAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imezitaka taasisi za serikali na mashirika yote ya umma kutumia Kituo cha Kutunzia Kumbukumbu cha Taifa chenye hadhi ya juu kabisa katika viwango vya ubora na usalama wa taarifa na kumbukumbu.

Pia imezitaka taasisi zote zilizo chini ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kutumia kituo hicho katika kutunza kumbukumbu zake ili kuwa mfano kwa taasisi nyingine za umma.


Akizungumzia maazimio ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu baada ya ziara ya siku moja ya kuitembelea Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) pamoja na miradi ya Mkongo wa Taifa na Kituo Mahiri cha Kutunzia Kumbukumbu, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Profesa Norman Sigala alisema uhai wa TTCL upo mikononi mwa serikali.

Aidha, Kamati hiyo ya Bunge imezitaka taasisi zote za umma na binafsi kulipa madeni inayodaiwa na TTCL kuiwezesha kampuni hiyo kujiendesha kwa ufanisi.

Mjumbe wa Kamati hiyo, Rita Kabati alisema kukamilika kwa mchakato wa kuondoka kwa Bharti Airtel ndani ya TTCL kunahitaji kwenda sambamba na uwezeshaji wa mtaji kama ilivyofanyika kwa Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) na Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) ambazo sasa zinafanya vizuri.
Chanzo:Habarileo.

Comments