Wakizungumza kwa nyakati tofauti mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, Nestory Baro washtakiwa hao walidai wamekuwa
wakizungushwa kutokana na mashauri dhidi yao kutokamilika hivyo kukaa muda mrefu mahabusu bila kesi ya msingi kusikilizwa.
Washtakiwa hao 61 wanaokabiliwa na mashtaka tofauti katika kesi 15, walidai wamekuwa wakiambiwa upelelezi haujakamilika, lakini wanaamini kinachofanyika ni kunyimwa haki zao za kikatiba.
“Ni mwaka wa nne sasa tangu tukamatwe na kesi tuliyopewa ni ya ugaidi, lakini tumekuwa tukizungushwa; tunakwenda, tunarudi na wimbo ni uleule wa upelelezi haujakamilika. Tumechoka kuzungushwa,” alidai mmoja wa washtakiwa mahakamani hapo.
Mwingine alidai: “Tumetengana na familia zetu, haziruhusiwi kutuona, mpaka sasa kesi ya msingi haijaanzwa kusikilizwa. Tunaitaka Serikali ituite pale itakapokuwa imekamilisha upelelezi na kama hawatakamilisha waamue, watoe taarifa kuwa tuko kizuizini kwa muda usiojulikana ili tukae mahabusu milele au tufe.
Tunataka upelelezi ukamilike haraka kesi ya msingi ianze lakini familia zetu ziruhusiwe kuja kutuona.”
“Tunatolewa kwa vitisho mji mzima unasimama tukipitishwa sisi, tunakuja tunapigishwa magoti, tunanyanyaswa watu wanaona na wanajua yanayotendeka lakini wameamua kukaa kimya,” alilalamika mshtakiwa mwingine.
Mshtakiwa mwingine alimuomba Rais John Magufuli kuingilia kati mwenendo wa kesi hiyo kwa kuwa inampotezea matumaini ya ndoto zake za kusoma.
Baada ya kusikiliza malalamiko yao, Hakimu Baro alisema atawasiliana na mkuu wa upelelezi wa makosa ya jinai Mkoa wa Arusha kuhusu tamko lao la kutohudhuria mahakamani.
Hakimu Baro alisema ni lazima wafike mahakamani Aprili 11 kesi itakapotajwa.
chanzoMwananchi.
Comments