Tanesco ‘yacheka’ wadaiwa kujisalimisha.

Kaimu Meneja Uhusiano wa Tanesco, Leila Muhaji SHIRIKA la Umeme Tanzania (Tanesco) limesema utaratibu wa kukusanya madeni kutoka kwa wadaiwa wake sugu na mwitikio wa kulipa madeni hayo unaendelea vizuri.

Hata hivyo, shirika hilo limesisitiza kuwa wale wote watakaokaidi kulipa madeni yao, litaendelea na utaratibu wake kuwakatia huduma ya umeme kama lilivyoahidi.


Hayo yalibainishwa Dar es Salaam na Kaimu Meneja Uhusiano wa shirika hilo, Leila Muhaji wakati alipozungumza na gazeti hili kwa njia ya simu kuhusu mwitikio wa wadaiwa wa Tanesco baada ya siku 14 zilizotolewa na shirika hilo kumalizika.

“Kwa sasa tunachofanya ni kukusanya taarifa kutoka kwa mameneja wa mikoa waliopewa kazi ya kusimamia utaratibu huo wa wanaolipa madeni yao,” alisema Muhaji na kufafanua kuwa, menejimenti ya shirika hilo imejipanga kuhakikisha kuwa wale wote ambao hawatatimiza wajibu wao na kulipa madeni yao, kukatiwa huduma za umeme.

“Pia tutatoa taarifa kuhusu mwitikio wa waliolipa pindi tutakapokamilisha kukusanya taarifa kutoka kwa vituo vyetu,” alieleza.

Machi 9, mwaka huu Tanesco ilitoa notisi ya siku 14 kwa wateja wake wote wanaodaiwa kulipa madeni yao, vinginevyo litawakatia huduma ya umeme wateja wote sugu wanaodaiwa na shirika hilo.

Shirika hilo linadai jumla ya Sh bilioni 275.38 na makundi yanayodaiwa ni pamoja na Wizara na Taasisi za Serikali zinazodaiwa zaidi ya Sh bilioni 52.53, Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO) linalodaiwa zaidi ya Sh bilioni 127.87 na kampuni binafsi pamoja na wateja wadogo ambao deni lao ni zaidi ya Sh bilioni 94.97.

Hata hivyo, tayari Serikali ya Zanzibar kupitia ZECO imeshapunguza deni lake na kulipa kiasi cha Sh bilioni 10 huku Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) likiahidi kulipa kiasi cha Sh bilioni moja kati ya zaidi ya Sh bilioni tatu linazodaiwa.

Hatua hiyo ya Tanesco kutoa siku 14 kwa wadaiwa wake sugu, imetokana na agizo la Rais John Magufuli wakati akizindua ujenzi wa mradi wa ujenzi wa kituo cha kupoza na kusambaza umeme wa kilovolti 132 mkoani Mtwara ambacho kitaboresha upatikanaji wa umeme kwenye Mikoa ya Mtwara na Lindi.

Katika agizo lake hilo kwa Tanesco alilitaka shirika hilo kuikatia umeme hata Ikulu endapo haitalipa deni la umeme, ili kuliwezesha shirika hilo kujiendesha zaidi.

chanzo:Mpekuziblog.

Comments