Serikali ya Sudan imeafiki suala la kuanzishwa njia ya amani kwa ajili ya kutuma misaada ya kibinadamu kwa watu walioathiriwa na ukame na njaa katika nchi jirani ya Sudan Kusini.
Kamishna wa Misaada ya Kibinadamu wa Sudan, Ahmed Mohamed Adam amesema kuwa serikali ya Khartoum
imekubali kuanzishwa njia ya amani ya kupitia katika miji ya El Obied katika jimbo la Kordofan kaskazini, Heglig jimboni Kordofan Kusini na Rubkona katika jimbo la Unity kwa ajili ya kupeleka misaada ya kibinadamu kwa watu wanaosumbuliwa na baa la njaa Sudan Kusini.
Njia hiyo itauwezesha Mpango wa Chakula Duniani (WFP) kupelekea misaada ya chakula katika majimbo ya Unity na Bahrul Ghazal.
Takwimu zinaonesha kuwa, katika mwezi uliopita wa Februari pekee Wasudan Kusini laki nne na 95 elfu wamekimbilia nchini Sudan kutokana na mapigano na njaa iliyoikumba nchi jirani ya Sudan Kusini.
Serikali ya Sudan Kusini inalaumiwa kwa kuchangia baa la njaa linaloshuhudiwa nchini humo wakati Rais wa nchi hiyo Salva Kiir akiendelea kutumia mamilioni ya dola zinazotokana na mauzo ya mafuta kuimarisha vikosi vyake vya ulinzi.
Vita vya ndani nchini humo vilivyoanza Disemba 2013 vimesababisha mauaji ya maelfu ya watu na kulazimisha mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi. Nchi hiyo ilitumbukia katika vita vya ndani baada ya Rais Salva Kiir kutoka kabila la Dinka kumtuhumu makamu wake wa zamani, Riek Machar wa kabila la Nuer kwamba alihusika na jaribio la kupindua serikali yake.
Hivi sasa Machar anaishi uhamishoni Afrika Kusini huku kukiwa na ripoti za uwezekano wa kuibuka mauaji ya kimbari katika nchi hiyo iliyojitenga na Sudan mwaka 2011.
chanzo:parstoday.
Comments