Moja ya mafanikio, Dk Shein alisema ni kutekeleza Ilani ya Uchaguzi
ya mwaka 2015-2020 katika miradi ya maendeleo na ustawi jami.
Dk Shein alisema hayo wakati alipofanya mazungumzo na waandishi wa
habari wa vyombo mbalimbali nchini ikiwa ni kutimiza mwaka mmoja na
kusisitiza kuwa Muungano hautavunjika na kero zake zitapatiwa ufumbuzi
kwa mazungumzo.
Alisema anajivunia mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha pili
kutokana na kushinda katika uchaguzi wa marudio wa Machi 20, 2016 ambayo
yameonesha njia ya kukua kwa uchumi na ustawi wa jamii huku sekta
binafsi ikishirikishwa kikamilifu katika ujenzi wa nchi miradi mikubwa
ya maendeleo.
Aliwataka wananchi kumuunga mkono katika mipango hiyo na kuwataka
kuachana na ndoto za baadhi ya wanasiasa wenye uchu wa madaraka ambao
wamekuwa wakipita na kuwadanganya wananchi kwamba wanasubiri kuingia
madarakani.
“Ninyi waandishi wa habari wakongwe na wale wanaochipukia mnajua
kwamba njia pekee ya kuwa rais katika nchi ni kushiriki katika
uchaguzi.....njia nyingine ni kufanya mapinduzi ambayo hayakubaliki
katika nchi za kidemokrasia,” alieleza.
Alijibu swali hilo wakati alipotakiwa kutoa ufafanuzi kama ipo
mipango inafanyika chini chini ya kuwepo kwa makubaliano kati yake na
Chama cha Wananchi (CUF) ikiwemo mazungumzo ya suluhu ya kisiasa.
Alisema hakuna mazungumzo ya kisiasa kati ya CCM na CUF yanayoendelea
sasa, kwani anafahamu kuwa uchaguzi umekwisha na serikali halali ipo
madarakani inafanya kazi kwa kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM.
“Mimi simzuii mtu kusema....... anayesema anajitayarisha kuapishwa
mwache aseme kwa sababu huo ni uamuzi wake na mdomo ni nyumba ya maneno,
lakini asivunje sheria za nchi tu,” alisema Dk Shein.
Aliongeza kwamba mafanikio makubwa yamepatikana katika kipindi cha
mwaka mmoja tu cha uongozi wake awamu ya pili ikiwemo kulipa pensheni ya
jamii kwa wananchi wote waliofikia umri wa miaka 70 ikiwemo wale ambao
hawajapata kuajiriwa na serikali.
Aidha, alisema serikali imefanikiwa kusimamia mapato katika vyanzo
vyake mbalimbali hatua imeifanya kulipa viinua mgongo kwa wafanyakazi
wastaafu wapatao 2,736 na kutumia Sh bilioni 38.
Alisema kwamba mafanikio yote hayo sasa yataiwezesha Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar kulipa mishahara mipya kwa wafanyakazi wake
kuanzia mwezi ujao ambapo kima cha chini kitaongezeka kwa asiimia 100.
chanzo:Habarileo.
Comments