Serikali ya China yaahidi kukamilisha jengo la abiria katika uwanja wa ndege wa Zanzibar.

SERIKALI ya Jamhuri ya Watu wa China imeahidi kukamilisha miradi yote inayoisaidia Zanzibar ikiwa ni pamoja na kukamilisha jengo jipya la abiria katika uwanja wa ndege wa Abeid Amani Karume haraka iwezekanavyo huku ikiahidi kuunga mkono ujenzi wa bandari mpya ya Mpigaduri.

Mjumbe wa Kamati Kuu na Katibu Mkuu wa Chama cha Kikomunisti cha China (CPC), Guo Jinglong
aliyasema hayo katika mazungumzo kati yake na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, huko Ikulu mjini Zanzibar.

Kiongozi huyo ambaye yuko ambaye yuko nchini, amempongeza Dk. Shein kwa juhudi zake za kuoingoza Zanzibar na kuweza kupiga hatua kubwa za maendeleo sambamba na kuimarisha amani na utulivu hapa nchini na kusisitiza kuwa hatua hiyo ya kuziunga mkono sekta hizo za maendeleo ikiwemo ujenzi huo wa jengo hilo jipya la abiria katyika uwanja wa ndege wa Zanzibar kutaimarisha sekta ya utalii.

Alisema kuwa tokea Dk. Shein kuweko madarakani Zanzibar imeendelea kupiga hatua kubwa za maendeleo na kuongeza kuwa kuchaguliwa kwake tena na wananchi kwa kipindi cha pili madarakani kuendelea na wadhifa wake huo kumezidi kuiletea maendeleo Zanzibar.

Kiongozi huyo alimueleza Dk. Shein kuwa Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China pamoja na chama chake cha CPC kimekuwa na uhusiano wa muda mrefu na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Kiongozi huyo wa CPC alimueleza Dk. Shein kuwa hakuna sababu ya kuvunjika kwa uhusiano huo uliopo na kueleza dhamira ya Serikali yake kuendelea kutoa ushirikiano kwa Zanzibar pamoja na kuendelea kukiunga mkono Chama Cha Mapinduzi.

Kuhusu sekta ya afya Kiongozi huyo alieleza kuwa China itaendelea na utaratibu wake wa kuleta madaktari hapa Zanzibar kwa kila baada ya muda uliopangwa ili kuimarisha utamaduni huo ambayo ulianzishwa tokea mwaka 1965.

Katibu Jinlong alisifu jitihada zinazoendelezwa na CCM ambazo zina itikadi zinazofanana na CPC hatua inayoonesha wazi ukomavu wa CCM kisiasa ambayo inawafanya wananchi walio wengi waendelee kukiamini chama hicho kutokana na Sera zake imara za maendeleo kwa ajili ya kuimarisha ustawi wa wananchi wa Tanzania bila ubaguzi.

Aidha, alieleza umuhimu wa viongozi wa vyama vya CCM na CPC kutembeleana ili kubadilishana mawazo na kuimarisha uhusiano na umoja wao wa kihistoria uliopo kati ya vyama hivyo.

Sambamba na hayo, Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya CPC alitoa pongezi kwa wananchi wa Zanzibar, Serikali na Chama Cha Mapinduzi kwa mapokezi mazuri waliyoyapata wakiwa hapa nchini yeye na ujumbe wake.

 Nae Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein alitumia fursa hiyo kutoa pongezi kwa ujio wa kiongozi huyo hapa nchini na kusisitiza kuwa hatua hiyo ni uhusiano mwema na ushirikiano uliopo kati ya CCM na CPC pamoja na Serikali za China na Tanzania.

Dk. Shein alisema kuwa azma ya China kuendelea kushirikiana na Zanzibar katika kuimarisha miradi ya maendeleo ukiwemo mradi wa ujenzi wa bandari ya Mpigaduri na uwanja wa ndege wa Abeid Amani Karume kutaimarisha ukuaji wa uchumi sambamba na kuimarisha sekta ya utalii.

Alieleza kuwa asilimai 80 ya fedha za kigeni zinatokana na mchango mkubwa wa sekta ya utalii ambayo pia, huchagia asilimai 27 ya pato la Taifa.

Aidha, Dk. Shein alisisitiza kuwa Zanzibar imekuwa na uhusiano na China tokea wa kihistoria kati yake na China hatua ambayo imewapelekea wananchi wa China kuweza kuishi Zanzibar na kuwa Watanzania hivi sasa.

Aliongeza kuwa Serikali ya China imeweza kuiunga mkono Zanzibar katika sektra mbali mbali za maendeleo ikiwemo sekta ya kilimo ambapo mara tu baada ya Mapinduzi matukufu ya Janurai 12, 1964 ambayo China ni miongoni mwa nchi za mwanzo kuyatambua ambapo pia, Serikali hiyo ilianzisha kilimo cha umwagiliaji maji hapa nchini.

Aidha, China ilijenga viwanda mbali mbali kikiwemo kiwanda cha sigara, kiwanda cha viatu pamoja na viwanda vidogo vidogo sambamba na kuleta wataalamu wa fani mbali mbali hapa Zanzibar.

Kwa upande wa sekta ya afya, Dk. Shein alisema kuwa serikali ya China imeweza kuunga mkono sekta ya afya kwa kuleta wataalamu wa sekta hiyo tokea mwaka 1965, na ujenzi mpya wa hospitali ya Abdalla Mzee pamoja na vifaa kwa hospitali hiyo na hospitali ya MnaziMmoja.

Sambamba na hayo, Dk. Shein alisisitiza kuwa hakuna jambo linaloweza kuondosha uhusiano wa kihistoria kati ya CCM na CPC pamoja na uhusiano wa Serikali zake ambapo alituma salamu za pongezi na kumtakia afya njema Rais wa China Xi Jinping na kupongeza hatua kubwa za maendeleo zilizofikiwa na nchi hiyo sambamba na kuimarika kwa uchumi wake.

 Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
 chanzo:zanzibar24.

Comments