Uchunguzi huo uliofanywa na tume iliyokuwa chini ya Mkemia Mkuu wa
Serikali, Profesa Samwel Manyele, umebainisha kuwa Faru John baada ya
kuhamishwa kutoka Ngorongoro na kupelekwa Sasakwa,
Grumeti alitelekezwa
na maofisa wa Hifadhi ya Ngorongoro kutokana na kutofuatilia maendeleo
ya afya ya mnyama huyo.
Aliitupia lawama Wizara ya Maliasili na Utalii na taasisi zake
zinazohusika na uhifadhi wa wanyamapori kuwa walichangia kifo cha Faru
John kutokana na kutofuata taratibu zilizowekwa kisheria na kuwepo kwa
mapungufu ya uongozi ndani ya taasisi hizo.
Alisema baada ya kupelekwa Grumeti, wahusika hawakurudi tena
kumwangalia na hivyo alipougua hakutibiwa.. Kwa hali hiyo tume hiyo
imeshauri serikali kuwachukulia hatua za wajumbe wote wa kamati ya
uongozi na wale wa Kamati ya Ufundi wa Hifadhi ya Ngorongoro.
Pia ripoti hiyo aliyokabidhiwa kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa,
imeishauri serikali kumchukulia hatua mtu aliyetajwa kwa jina moja la Dk
Kileo wa Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (Tanapa) kwa kuwa ndiye alikuwa na
jukumu la kuhakikisha Faru John anakuwa na afya nzuri, lakini badala
yake alimtelekeza huko Grumeti.
Uthibitisho wa kifo
Profesa Manyele alisema sampuli 45 zilichukuliwa kwenye mzoga wa Faru
huko Sasakwa, Maabara ya Hifadhi ya Ngorongoro na Chuo Kikuu cha Kilimo
cha Sokoine (SUA), sampuli za uchunguzi kutoka Taasisi ya Wanyamapori
(TAWIRI) na Tanapa.
Alisema pia walichukua kipande cha pembe cha Faru John kilichokatwa
wakati wa kumwekea ‘transmitter’ na ambacho hakikuwasilishwa kwa Waziri
Mkuu, sampuli za pembe mbili kutoka hifadhi ya nyara iliyoko Dar es
Salaam.
Alitaja aina ya sampuli hizo kuwa ni mifupa ambayo ni fuvu na mzoga
uliokuwa Sasakwa Grumeti, pembe mbili zilizochukuliwa Dar es Salaam na
pembe moja iliyochukuliwa Ngorongoro, damu kutoka maabara ya Ngorongoro
na SUA, ngozi kutoka kwenye mzoga Sasakwa na kinyesi kilichokaushwa
kutoka SUA.
Alisema baada ya sampuli hizo kupelekwa Afrika Kusini katika Chuo
Kikuu cha Pretoria, maeneo ya ulinganishaji wa vinasaba na mfanano
ulikuwa asilimia 100.
“Mzoga, fuvu, pembe zote tatu, damu zote ni za faru John. Pembe
alizowasilisha Waziri wa Maliasili na Utalii zilikuwa za Faru John, damu
zilizokusanywa zilikuwa za Faru John...Faru John alikufa Sasakwa,
Grumeti,” alisema Profesa Manyele.
Licha ya sampuli, tume hiyo iliwahoji watumishi na watu wengine wapatao 18 ambao pia walithibitisha kifo cha Faru John.
Matokeo ya uchunguzi
Alisema licha ya kuwepo mawasiliano kati ya wizara na taasisi zake,
hapakuwepo na kibali rasmi kutoka kwa Mkurugenzi wa Wanyamapori cha
kuruhusu kumhamisha Faru John kutoka Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro
(NCAA) kwenda Grumeti.
Tume hiyo imeshauri hatua za kinidhamu zichukuliwe dhidi ya Ofisi ya
Mkurugenzi wa Wanyamapori na Mhifadhi wa NCCA kutokana na mapungufu ya
kiutendaji ya kuruhusu Faru John kuondolewa bila kibali.
“Tume inashauri taratibu za kuhamisha wanyama walio katika hatari ya
kutoweka ziwekwe bayana, zianishe kwenye ikanuni na sheria,” alieleza
Manyele na kuongeza kuwa, tume hiyo ilibaini kutokuwepo na mkataba rasmi
kati ya serikali na mwekezaji unaonesha mnyama ametoka serikalini na
kwenda kwa mwekezaji.
Migogoro ya wafanyakazi
Uchunguzi huo pia ulibaini kuwa wakati wa sakata hilo la Faru John,
NCCA iliingia kwenye migongano na baadhi ya wafanyakazi wake ambao
walikuwa wanasimamia maslahi ya taifa katika kuhifadhi wanyamapori.
Alishauri serikali iunde tume huru kuchunguza migogoro ya kimaslahi
kati ya watumishi wa NCCA dhidi ya uwekezaji ndani ya hifadhi na hatua
stahiki zichukuliwe.
“Tunashauri serikali ifanye tathmini ya kina kuona kama uongozi
uliopo kwa sasa NCAA unajitosheleza kuendelea kuongoza taasisi hiyo kwa
maslahi mapana ya taifa,” alisema Profesa Manyele.
Ongezeko la mifugo, watu
Tume hiyo pia ilionya kuwa ongezeko la watu ambalo kwa sasa linafikia
watu 90,000 walioko kwenye hifadhi ya NCAA kutoka watu 8,000 mwaka 1959
ni mwanya wa majangili kujipenyeza na kujificha.
Alisema ni hatari kwa baadhi ya wanyama kutoweka na kupotea. Tume
imeshauri tathmini ya kina ifanyike ili kubaini athari zinazojitokeza
kutokana na ongezeko la watu na mifugo NCCA.
Alisema sheria hiyo ipitiwe upya na kuona umuhimu wake kwa sasa.
Uwekezaji hatari
Katika ripoti yake alisema uwekezaji uliofanywa ndani ya Hifadhi ya
Ngorongoro ni hatari kutokana na maamuzi yake kufanywa na wizara peke
yake.
Alisema matokeo yake uwekezaji wa ujenzi wa Ndutu Lodge umefanywa
katika maeneo ya mapitio ya wanyama na ujenzi huo ulifanyika bila
kufanyika kwa Tathmini ya Athari za Kimazingira (EIA).
Imeshauri ujenzi wa Ndutu Lodge uchunguzwe upya. Pia uchunguzi wa aina hiyo ufanyike kwenye maeneo mengine ya hifadhi za taifa.
Udhibiti wa ujangili
Alisema tume yake inashauri kufanyike utambuzi wa wakazi halali ndani
ya kreta ya Ngorongoro na maeneo mengine ya Serengeti na kuzuia
uhamiaji katika maeneo hayo.
Pia ameshauri kuanzishwa na kuimarisha maabara ya DNA ya wanyama
chini ya maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali ili kutoa msaada kwa vyombo
ya haki jinai katika kupeleleza na kuchunguza kazi zinazohusiana na
ujangili.
Wameshauri pia kuimarisha vikosi vya kuzuia ujangili kwa kushirikisha jeshi la wananchi, kwa namna itakavyoonekana inafaa.
Lakini wameonya pia kuwa mwingiliano kati ya mifugo na wanyamapori
kunatoa mwanga wa majangili kutumia nafasi hiyo kufanya uhalifu. “Tume
inashauri kuwepo udhibiti wa sheria kali ya kuzuia mifugo katika maeneo
ya hifadhi,” alisema.
Aliongeza kuwa vibali vya uwindaji vya wanyama wanaoelekea kutoweka vifutwe. Sheria ipitiwe ili kuzuia vibali hivyo.
Viwanja vya ndege vilivyopo ndani ya hifadhi vifanyiwe tathmini ya
kina juu ya manufaa ya uwepo wake, usimamizi na uendeshaji wake ili
kulinda maslahi ya taifa.
Alisema Wizara ya Maliasili na Utalii ilipuuza maoni ya wataalamu
wakati wa kufanya maamuzi. Pia tume hiyo imekosoa maamuzi makubwa ya
kitaifa kufanywa na mkurugenzi wa wanyamapori peke yake.
Kauli ya Waziri Mkuu Waziri Mkuu Majaliwa alisema Serikali
itayafanyia kazi mapendekezo yote yaliyotolewa na tume hiyo na
kuyatangaza kwa umma.
“Ripoti hii ni ndefu sana, ngoja tukaisome, matokeo tutakayochukua tutayatangaza kwa umma,” alisema Majaliwa.
chanzo:Habarileo.
Comments