RC: Msikubali kutumika kwenye migogoro ya ardhi.

Polisi wakiwatuliza wananchi waliokuwa wamezuia Kamati iliyoundwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa inayoongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo kuendelea na kazi yake ya kuhakiki maeneo muhimu yaliyopo ndani ya Pori Tengefu la Loliondo, katika Kata ya Ololosokwan wilayani Ngrongoro mkoa wa Arusha ambapo walikataa kuhamishwa kwenye eneo hilo. (Picha na Veronica Mheta).BAADHI ya wanawake na watoto wanatumiwa kama chambo kwa ajili ya kusimamisha msafara wa Kamati ya kukamilisha mchakato wa utatuzi wa mgogoro wa matumizi ya ardhi kwenye pori tengefu la Loliondo.

Kutumika kwa wanawake hao ambao baadhi yao walikuwa na watoto wadogo migongoni kumebainika jana wakati kamati hiyo ilipokuwa ikiendelea kuangalia maeneo mbalimbali ya pori hilo tengefu la Loliondo lenye ukubwa wa kilomita 15,000 za mraba zilizoleta mgogoro kwa zaidi ya miaka 25 sasa.


Wanawake hao katika Kata ya Malambo na Kata ya Arash, walibeba mabango ya kuisihi kamati hiyo kutenda haki, huku mengine yakimtuhumu Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe kuwapenda wanyamapori kuliko binadamu.

Baadhi ya wanawake hao ambao ni Rehema Pascal na Lemnyaki John walisimamisha msafara huo kwa kuonesha mabango yao yanayodai kutokubali kuhamishwa katika pori hilo huku wengine wakipandisha mori na kupiga mayowe.
Baada ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo kuyasoma mabango hayo aliwapa vipaza sauti ili wayasome tena, hapo ndipo waliposhindwa kuyasoma na kudai kuwa hawajui Kiswahili.

“Nani aliyewaandikia mabango haya wakati hamjui kusoma, mnatumiwa na viongozi wenu kuhusu mgogoro huu, msikubali kutumika maana hamjui serikali inafanya hivi kwa nia ipi na wala serikali haina mpango wa kuchukua ardhi hii bali tunachokifanya ni kujua hayo mnayoyasema yapo kiuhalisia au la ili tukamilishe kazi yetu,” alisema Gambo.

Naye Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Felix Wandwe, aliwataka wananchi wa kata saba za wilaya hiyo kutokubali kutumika vibaya kwa ajili ya pori hilo, kwani serikali inachofanya hivi sasa ni kuchukua mapendekezo ya kamati hiyo kisha kuyawasilisha kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Pia, Katibu wa Kamati hiyo, Bahati Chisanza, alisema kuwa ni vyema wananchi wakajua kuwa serikali haichukui ardhi bali inachokifanya ni kutaka kupanga matumizi bora ya ardhi ili kila mtu anufaike nayo.

Awali, Mwenyekiti wa Kijiji cha Malambo, Lazaro Mashele alitoa rai kwa kamati hiyo kutoiingiza kata hiyo ya Malambo katika matumizi bora ya ardhi, kwani kata hiyo haina mgogoro na pori hilo bali ni wahifadhi wazuri wa wanyamapori ingawa kata hiyo ni sehemu ya mazalia ya wanyama.

“Tunawaomba wakuu kata hii isiingizwe katika mgogoro huu kwani hatupo ndani ya vijiji saba lakini pia kata hii inatumika kwa ajili ya mazalia ya wanyamapori ambao hatuna ugomvi nao”.

Kwa upande wake, Gambo alisisitiza kuwa kamati hiyo imechukua maoni ya mwenyekiti huyo na watafanyia kazi maoni yote yaliyotolewa na wananchi, wahifadhi na wataalamu wa ardhi kisha kuyawasilisha kwa Waziri Mkuu Machi 25, mwaka huu.
chanzo:Habarileo.

Comments