Ndugu wawili wajeruhiwa na chui wakimuokoa ndama.

NdamaNDUGU wawili wa familia moja, Maiko Joseph (27) na mdogo wake, Njamili Karatasi (22) wamejeruhiwa vibaya na chui dume aliyekuwa wakipambana naye kwa nyakati tofauti baada ya mnyama huyo kuingia ndani ya zizi la baba yao mzazi Joseph Maiko na kuwashambulia ng’ombe.

Wawili hao ambao ni wakazi wa Kijiji cha Katambike katika Kata ya Ugala wilayani Mpanda mkoani Katavi, wamelazwa katika Hospitali ya Manispaa ya Mpanda kwa matibabu.


Akizungumzia mkasa huo, Diwani wa Kata ya Ugala, Halawa Malendeja alisema shambulio hilo lilifanyika juzi saa 12 alfajiri, baada ya chui kuiingia kwenye zizi la ng’ombe nyumbani kwa Joseph Maiko ambaye ni baba mzazi wa wawili hao.

“Baada ya chui huyo kuingia zizini alimshambulia ndama wa ng’ombe, akiwa katika harakati ya kuondoka na ndama huyo ili akamle nje ya zizi hilo…. ndipo Njamila aliposikia purukushani hizo zilizomsukuma atoke nje ya nyumba alimokuwa amelala na kwenda kwenye eneo la tukio na kushuhudia chui huyo akitaka kutoka nje ya zizi hilo akiwa na ndama huyo,” alieleza Malendeja.

Aliongeza kuwa ndipo Njamili alipoingia zizini na kuanza kumshambulia chui huyo kwa rungu na mnyama huyo alimwachia ndama aliyekuwa anamburuza ili amtoe nje ya zizi hilo na kuanza kumshambulia Njamili ambaye alipoona amezidiwa, alianza kupiga mayowe akiomba msaada.

Inadaiwa kuwa kaka yake Njamili, Maiko alisikia mdogo wake akipiga kelele akiomba msaada ndipo alipotoka nje ya nyumba kwenda eneo la tukio akiwa na rungu mkononi.

“Maiko aliingia zizini na kuanza kumshambulia chui huyo kwa rungu ili kumuokoa mdogo wake ….. 
mnyama huyo alimwacha mdogo wake akiwa tayari amemjeruhi vibaya mkono wake wa kulia uliokuwa ukivuja damu nyingi na kumrukia Maiko na kumuuma shavu la kulia na kumjeruhi vibaya,” aliongeza diwani.

Kwa mujibu wa diwani huyo, Maiko licha ya kung’atwa shavuni, alionesha ujasiri mkubwa kwa kuikamata miguu ya mbele ya mnyama huyo na kumwangusha chini na kuendelea kumshikilia.
Wakati akiendelea kupambana na chui, Njamili aliendelea kupiga mayowe kwa kwa nguvu, ndipo majirani walipofika na kumuua chui huyo.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Katavi, Damas Nyanda akithibitisha kutokea kwa shambulio hilo na alieleza kuwa majeruhi hao wawili walikimbizwa na kulazwa katika Zahanati ya Ugala kwa matibabu, ambako walipatiwa huduma ya kwanza kisha wakahamishiwa Hospital iya Manispaa ya Mpanda kwa matibabu zaidi.

Akizungumza akiwa hospitalini, Njamili alidai kuwa chui huyo alikuwa dume, na licha ya kumparua sehemu mbalimbali za mwili wake, pia alimjeruhi vibaya mkono wa kulia.
chanzo:Habarileo.

Comments