Akizungumza wakati wa akikaribishwa ofisini mjini Dodoma, Waziri wa
Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe alisisitiza
umuhimu wa Watanzania kuhamasisha matumizi ya Kiswahili.
Katika mabadiliko makubwa atakayofanya wizarani ni pamoja na
kuhakikisha Kiswahili kinapewa msukumo wa aina yake, hasa baada ya Rais
John Magufuli kuonesha njia ya kuzungumza lugha hiyo katika mikutano
mbalimbali ya ndani na nje ya nchi.
Dk Mwakyembe alimpongeza Rais Magufuli kwa kuhamasisha na kuzungumza
Kiswahili katika mikutano mbalimbali, akisema kiongozi huyo wa nchi
ameonesha njia, hivyo wananchi wanatakiwa kuifagilia na kuifuata kwa
kuhamasisha Kiswahili.
“Rais Magufuli ameonesha dhamira ya dhati ya kukuza Kiswahili, sisi
hatuna budi kukifagilia na kuhamasisha matumizi ya lugha hiyo,” alieleza
Dk Mwakyembe ambaye jana alikaribishwa wizarani hapo baada ya uteuzi
wake wa hivi karibuni akitokea Wizara ya Katiba na Sheria.
Alisema kiongozi huyo anatumia lugha hiyo namba moja nchini, kwenye
mikutano ya ndani na ya kimataifa, hivyo wengine wanatakiwa kuiga mfano
huo wa kuitumia.
Dk Mwakyembe alisema alipomuuliza Katibu wa Wizara, Profesa Elisante
ole Gabriel, nafasi ya Kiswahili duniani, alidhani kwamba angesema ni ya
200 hivi, alishangaa kusikia kwamba ni lugha ya 10 kwa umaarufu
duniani.
“Tunatakiwa kujifunza Kiswahili kutokana na ukweli kwamba kujifunza
au kuzungumza kwa kutumia lugha kama Kiingereza inakuwa taabu,” alieleza
na kuongeza kuwa atazungumza na viongozi wa Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki kuona ni namna gani Kiswahili kitapewa
msukumo wa kutosha na kutumika zaidi katika maeneo na mikutano
mbalimbali.
chanzo:Habarileo.
Comments