Msalaba Mwekundu: Dunia ina miezi 3 kunusuru mamilioni wanaokabiliwa na njaa Somalia, Yemen.

Shirika la Msalaba Mwekundu limeonya kuwa, jamii ya kimataifa ina miezi mitatu hadi minne kuokosoa maisha ya mamilioni ya watu wanaokabiliwa na baa la njaa katika nchi za Somalia na Yemen.

Dominik Stillhart, Mkurugenzi wa Operesheni za Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu amesema kuwa, iwapo hatua za dharura hazitachukuliwa katika kipindi hicho, mamilioni ya raia wa Somalia na Yemen watapoteza maisha kutokana na njaa.


Akiongea na waandishi wa habari mjini Geneva, afisa huyo wa Msalaba Mwekundu amesema shirika hilo linahitaji dola milioni 300 za Marekani kwa ajili ya msaada wa chakula kwa watu wanaokabiliwa na baa la njaa lililosababishwa na ukame katika nchi mbili hizo.

Ameongeza kuwa, watu milioni 20 hususan wanawake na watoto wadogo wapo katika hatari ya kufa njaa katika nchi hizo, pamoja na Sudan Kusini na Nigeria.

Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu imesema kuwa, kufikia sasa, imepokea dola milioni 100 za Marekani pekee kati ya milioni 400 inazohitaji ili kushughulikia hali hiyo ya kibinadamu katika nchi hizo tatu za Afrika na Yemen.

Taasisi hiyo ya kimataifa imekumbusha kuwa, iwapo jamii ya kimataifa itajikokota katika kulishughulikia janga hili, yumkini mamia ya maelfu ya watu watapoteza maisha katika nchi hizo kama ilivyoshuhudiwa miaka ya nyuma. Itakumbukwa kuwa, mwaka 2011, watu zaidi ya laki 260 walikufa njaa nchini Somalia.
chanzo: parstoday.

Comments