Mradi huo wa kuzalisha na kusambaza umeme katika maporomoko ya maji
ya Rusumo katika Mto Kagera utanufaisha nchi tatu za Tanzania, Rwanda na
Burundi.
Ujenzi wa mtambo wa kuzalisha umeme unagharimiwa na Benki ya Dunia
ilhali ujenzi wa njia ya umeme kuunganisha katika Gridi za Taifa za nchi
hizo tatu unafadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), kwa
mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na waandalizi wa
uzinduzi huo.
Wadau wengine wanaotarajiwa katika uzinduzi ni wawakilishi kutoka
Benki ya Dunia, AfDB na wajumbe wa Bodi ya Mradi wa Umeme wa Rusumo
kutoka nchi hizo tatu.
Kupitia kwa mpango huo kabambe, kila nchi itapata nyongeza ya
megawati 26.6 katika gridi zao za taifa na hili linatarajiwa pia
kuimarisha uunganishwaji umeme wa kikanda baina ya nchi hizo tatu ambazo
pia ni wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
“Kukamilika kwa mradi huu kutanufaisha kaya elfu saba (7,000) kupitia
mpango wa maendeleo katika serikali za mitaa na kaya nyingine 188
zinazozunguka mradi huu,” ilisema taarifa hiyo na kuongeza kuwa
inategemewa pia wakati wa utekelezaji wa mradi huu kabambe wa kikanda
katika eneo la Afrika Mashariki, kutakuwa na ajira kwa zaidi ya
wafanyakazi 500 wenye weledi, weledi wa kati na vibarua kutoka nchi tatu
zitakazonufaika na mradi huu.
Ujenzi wa mradi unatarajiwa kutekelezwa kwa miaka mitatu na
utakamilika mwaka 2020.
Makandarasi wawili kutoka China, CGCOC Group Ltd
na Jiangxi Water & Hydropower Construction Company Ltd (CGCOC -
JWHC JV) watajenga bwawa la maji pamoja na miundombinu mingine.
Kwa upande mwingine, muunganiko wa makandarasi wawili Rusumo Falls
Andritz Hydro GmbH ya Ujerumani na Andritz Hydro PVT Ltd ya India
watahusika na ufungaji wa mitambo ya kuzalisha na kusambaza umeme.
Mradi wa kuzalisha umeme wa maji wa Rusumo unasimamiwa na taasisi ya
Nile Equatorial Lakes Subsidiary Action Program Co-ordination Unit
(NELSAP-CU) iliyopewa jukumu hilo na nchi tatu wanufaika kupitia Kampuni
ya Rusumo Power Ltd (RPCL), inayomilikiwa kwa pamoja na mashirika ya
umeme katika nchi za Tanzania, Rwanda na Burundi.
chanzo:Habarileo.
Comments