Aidha, wakurugenzi na wenyeviti wa bodi wa mashirika hayo kuanzia
mwakani watatakiwa kuwasilisha bajeti zao bungeni ili kupitishwa na
Bunge na hakuna shirika lolote la serikali litakaloweza kupitishwa
bajeti bila kuidhinishwa na Bunge.
Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti wa kamati hiyo, Albert Ntabaliba
wakati kamati hiyo ilipotembelea miradi ya Kituo cha Kimataifa cha
Mikutano (AICC) na kujionea miradi mbalimbali inayoendeshwa na kituo
hicho, ikiwemo ujenzi wa nyumba za kupangisha, hospitali na jengo la
maonesho na mikutano linaloendelea kujengwa na kituo hicho.
Ntabaliba alisema licha ya mashirika hayo kuwa na thamani kubwa ya Sh
trilioni 26, lakini yamekuwa hayachangii ipasavyo bajeti ya serikali,
hivyo yanatakiwa yabadilike na kuanza kulipa kodi ipasavyo pamoja na
kutoa gawio serikalini.
“Mashirika yote ya umma yaliyopo nchini yana thamani ya shilingi
trilioni 26 na kwa mwaka yamekuwa yakitoa faida ya shilingi bilioni 450
pekee, ambayo ni sawa na asilimia 1.08 kitu ambacho hakiwezekani
ukilinganisha na mtaji uliopo wa trilioni 26, na hivyo wakurugenzi na
wenyeviti wa bodi wametakiwa wahakikishe mapato yao kwa serikali
yanapanda na angalau waweze kuchangia trilioni mbili kwa mwaka,” alisema
Ntalibaliba.
Akizungumzia AICC, alipongeza miradi inayoendeshwa na kituo hicho na
kushauri waanze kuchukua hatua ya kuanza kukabiliana na soko na pia
wajitahidi kuwekeza zaidi katika ujenzi wa vituo vya mikutano vya kisasa
na kuwataka kuelekeza nguvu zaidi ya kujenga kituo kikubwa cha mikutano
katika mji mkuu wa Tanzania ambao ni Dodoma.
Hata hivyo, mmoja wa wabunge wa kamati hiyo, Ester Bulaya alikosoa
gharama za ukarabati zilizotumika kukarabati Ukumbi wa Simba katika
kituo hicho ambao kiasi cha Sh bilioni tatu na nusu zilitumika jambo
ambalo hawakuafiki na kushauri kwamba fedha hizo ni nyingi sana na
zingeweza kutumika kwenye uwekezaji mwingine.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa AICC, Elishilia Kaaya alisema
amefurahishwa na ujio wa kamati hiyo kuwatembelea na pia wamekutana nao
na wamepewa elimu nzuri ya uwekezaji na wametazama baadhi ya mambo yale
ambayo hayajaenda sawa wamewarekebisha pale ambapo awapo vyema
wamewafundisha hivyo wanaamini walivyoambiwa mtazamo ubadili utabadilika
kulingana na hali ilivyo.
Hata hivyo, alisema kwa sasa wameanzisha mradi ujenzi wa kumbi za
mikutano, mahoteli na maonesho unaogharimu Sh bilioni 2.8, ambao
unatarajiwa kukamilika Mei mwaka huu, ambapo wanategemea utasaidia
kuongeza mapato ya kituo hicho pamoja na ajira kwa Watanzania.
chanzo:Habarileo.
Comments