Mapendekezo ya washiriki wa mkutano wa marekebisho ya sheria za fidia na ile ya usalama kazini.

Washiriki wa mkutano wa marekebisho ya sheria za fidia na ile ya usalama kazini, wamependekeza katika marekebisho ya sheria hizo, kuwe na kitendo maalumu ndani ya mahakama ya Mkoa, inayoshughulikia upatikanaji wa fidia, pale wafanyakazi wanapopata ajali wanapokuwa kazini.
Walisema suala la fidia kumtaka mfanyakazi aliepata ajali au kuumia kazini,
shauri lake liwemo kwenye mahakama za kawaida, ni kumuomgezea maumivu kutokana na mahakama hizo kuzidiwa na kesi.
Washiriki hao walieleza hayo kwenye skuli ya sekondari Madungu na ofisi ya mkuu wa wilaya ya Mkoani, wakati Tume ya kurekebisha sheria ilipokutana na wajumbe hao, kuomba mapendekezo yao ili kuzifanyia marekebisho sheria za fidia na ile ya usalama kazini.
Washiriki hao, walisema ili haki za fidia kwa mfanyakazi iwe rahisi kupatikana, ni vyema ndani ya mahakama za mkoa kuwe na kitengo maalum, ili kurahisisha hukumu ya kesi yake.
Mussa Khamis Mussa alisema, haiwi busara kuona mfanyakazi amepata ajali, kisha haki yake kuidiai kwenye mahakama ya Mkoa, ambazo imezidiwa na rundo la kesi.
Nae Afisa utumishi kutoka baraza la mji Chakechake Khadija Haroun Bakar alisema, kwanza lazima sheria za kazi na fidia zifundishwe kwa wafanyakazi, kisha kuwe na kitengo cha kudai haki zao.
“Tunayo mahakama ya ardhi, mahakama ya kazi, bali na hili la fidia liandaliwe kitengo chake, ili kuwarahisishia wafanyakazi wanaotaka kukata rufaa au kudai haki’’,alifafanua.
Wakiwasilisha mapendekezo ya sheria hizo, wanasheria kutoka Tume ya Kurekebisha Sheria Zanzibar, Ali Juma Ali na Mohamed Ali Ahmed walisema, pia sheria hizo hazikumpa haki mteule wa rais katika ukataji wa rufaa.
Walisema hata hivyo, sheria hizo hazijakidhi hadhi ya mahitaji ya kimataifa, sambamba na kuacha kutaja iwapo mfanyakazi amepata ajali ya kutoka meno au pua hakuna maelekezo ya fidia.
“Sheria imetaja ukikatika mguu, mkono, kupofua jicho moja au yote mawili na kupata athari ya mavumbi, lakini imesahau viungo kama pua, meno, sikio sasa lazima na haya yamemo’’,alisema Ali Juma Ali.
Sheria ambazo Tume ya Kurekebisha Sheria Zanzibar inazifanyia mapitio ni ile sheria ya fidia ya kazini no 15 ya mwaka 1986 pamoja na marekebisho yake ya mwaka 2005 na sheria ya usalama kazini no 8 ya mwaka 2005.
chanzo:zanzibar24.

Comments