Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam, Waziri wa Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alisema
serikali inawatoa hofu madaktari hao juu ya usalama wao na kwamba
waendelee kuomba nafasi hizo.
“Madaktari wetu hawa tunawatoa hofu wasiwe na wasiwasi kuhusu usalama
wao wakifanya kazi nchini humo kwani Rais Uhuru Kenyatta ambaye ni
mwenyeji wetu amemhakikisha Rais John Magufuli kuwa watakuwa salama
wakati wote,” alisema Ummy.
Hivi karibuni, Rais John Magufuli aliridhia ombi la Rais Uhuru
Kenyatta wa Kenya kwa kuruhusu madaktari 500 nchini kwenda kufanya kazi
nchini Kenya, baada ya nchi hiyo kukumbwa na mgomo wa madaktari.
Waziri Ummy alisema imeandaliwa rasimu ya makubaliano kati ya
Tanzania na Kenya ili kuhakikisha hayo yanasimamiwa kwa dhati na mambo
waliyoahidiwa yanatekelezwa ikiwemo maslahi ya madaktari hao.
“Tunatarajia kutumia siku mbili serikali ya Tanzania na ya Kenya,
kupitia rasimu hiyo na Machi 24, mwaka huu nitawasiliana na Waziri wa
Afya wa Kenya ili tushauriane katika upungufu tutakaokuwa tumeubaini
kabla hatujaweka saini Machi 27, mwaka huu,” alifafanua waziri huyo.
Aidha, alisema wadau mbalimbali wa sekta ya afya watahusishwa ili kupata maoni yao wakiwamo Chama cha Madaktari Tanzania (MAT).
Alikiri pia kuwa sekta ya afya kwa ujumla ina upungufu wa watumishi
kwa asilimia 51 na kwamba upungufu huo sio wa madaktari pekee, bali
watumishi wa sekta nzima.
“Tumewasiliana na wenzetu Utumishi na Wizara ya Fedha kuhusu ajira,
lakini hatuwezi kuwaajiri madaktari hao wote 2,700 ambao wanazalishwa
kila mwaka, mwaka huu tutaajiri, lakini tutaajiri madaktari 500 tu,”
alibainisha Ummy.
Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Mohamed Bakari alisema serikali zote
mbili zilijadili ajira hizo na faida zake kwa madaktari wa Tanzania na
kwamba hiyo ni fursa za ajira kwa madaktari na pia itasaidia kuimarisha
uhusiano baina ya Tanzania na Kenya.
“Madaktari 1,764 wanahitimu katika vyuo vya afya 11 vilivyopo nchini
kila mwaka, mwaka huu tunatarajia idadi hiyo itaongezeka hadi kufikia
madaktari 2,843, imekuja fursa hii ambayo tunaona itatupunguzia mzigo,”
alisema Dk Bakari.
Alisema madaktari watakaokwenda nchini Kenya watapata uzoefu wa
kufanya kazi nje ya nchi na kwamba kwa nyakati tofauti Tanzania imekuwa
tukipokea madaktari kutoka katika mataifa mengine ikiwamo Kenya yenyewe.
Katika hatua nyingine, Waziri Ummy ametangaza kuwa wizara hiyo
imefuta aina 20 za vinywaji vya pombe kali zilizofungashwa katika
plastiki maarufu viroba.
Aidha, agizo hilo pia ni pamoja na kusitisha utoaji wa vibali vya
viroba kwa pombe kali zilizofungashwa kwenye chupa zilizo na ujazo wa
chini ya mililita 200 na kwamba usitishwaji huo umeanza rasmi Machi mosi
mwaka huu.
Akifafanua agizo hilo, Ummy alisema Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA)
ilikuwa imesajili aina 20 za vinywaji vya pombe kali vilivyofungashwa
kwa namna hiyo na kati ya hizo aina tano muda wake wa usajili ulikuwa
umekwisha.
“Uamuzi wa kupiga marufuku matumizi ya pombe hiyo, unatokana na
athari mbalimbali zikiwamo za kiafya na kijamii, matumizi ya pombe hizi
yamesababisha ajali nyingi, vifo, ulemavu na ni mzigo mkubwa kwa
serikali katika tiba za magonjwa,” alisema.
Alisema uamuzi huo ni kwa mujibu wa Kifungu cha 25 (1) cha Sheria ya
Chakula, Dawa na Vipodozi, Sura 219 na kwamba kwa mujibu wa kifungu cha
20(2)(b)(2) cha sheria hiyo matumizi ya pombe hizo hayana tija kwa
Taifa.
Alisema wizara hiyo inasubiri maelekezo kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu
kujua iwapo vile viroba vilivyokamatwa viteketezwe au virudishwe
viwandani ili vikafungashwe upya katika ujazo unaofaa.
Awali alipozungumza katika uzinduzi wa Bodi ya Taasisi ya Jakaya
Kikwete, Waziri Ummy alisema pia kuwa watu wengi wanaoenda nje ya nchi
kwa ajili ya matibabu ya saratani ni kwa ajili ya kipimo, hivyo serikali
katika bajeti ijayo imetenga Sh bilioni 50 kwa ajili ya kununua mashine
ya kipimo hicho.
“Maana yake Tanzania itakuwa ya kwanza ukanda huu wa Afrika Mashariki
kuwa na kipimo hicho, kama tunavyojua wanavyoenda sio kwamba wanaenda
kupata tiba, wanaenda kufanya kipimo, zaidi ya wagonjwa wa kansa
wanaoenda nje ya nchi tutawapunguza kwa asilimia 50,” alisema Ummy.
Aidha, alisema serikali inadaiwa zaidi ya Sh bilioni 30 na hospitali
za India ambazo zinawatibu wagonjwa wenye matatizo ya moyo wanaopelekwa
na serikali na kwamba hospitali hizo zinakaribia kusitisha huduma
kutokana na deni hilo.
“Acha niwe mkweli, fedha hizo tunatumia kulipa madeni, tunadaiwa
zaidi ya bilioni 30, fedha kweli napata, lakini nadaiwa na hospitali za
India tunazopeleka wagonjwa wetu,” alisema na kuahidi kuwa fedha
zikitengwa kwa ajili ya matibabu nje ya nchi zitakuwa zinasambazwa
Muhimbili, Taasisi ya Mifupa Moi na taasisi hiyo ya JKCI na Ocean Road.
chanzo:Habarileo.
Comments