Shirika la Kimataifa la Wahamiaji lilitangaza habari hiyo jana na kuongeza kuwa, maafisa wawili wa kutoa misaada ya kibinadamu wameuawa na wengine watatu kujeruhiwa baada ya msafara wao kushambuliwa na watu wenye silaha.
Shirika hilo limesema, hii si mara ya kwanza kwa wafanyakazi wa mashirika ya misaada ya kibinadamu kushambuliwa na makundi yenye silaha na kuporwa misaada wanayowapelekea raia huko Sudan Kusini.
Mwezi uliopita, Umoja wa Mataifa ulitangaza kuwa, baadhi ya maeneo ya Sudan Kusini yamekumbwa na ukame na inatathminiwa kuwa karibu nusu ya raia wa nchi hiyo yaani takriban watu milioni tano na nusu wanahitajia mno misaada ya chakula.
Sudan Kusini ilitumbukia kwenye machafuko tangu mwaka 2013 baada ya Rais Salva Kiir kumtuhumu makamu wake wakati huo, Riek Machar, kwamba alikuwa na nia ya kumpindua.
chanzo:parstoday.
Comments