Kwa mujibu wa shirika la habari la IRNA, Abdul Fattah Halanah, mmoja wa maafisa wa ngazi za juu wa masuala ya usalama nchini Somalia amesema,
vikosi vya nchi hiyo vimefanya operesheni maalumu katika eneo la Suka-Holaha karibu na Mogadishu na kufanikiwa kugundua maficho ya Ja'far Kukay, mmoja wa viongozi waandamizi wa kundi la al Shabab na baadaye kumwangamiza.
Amesema, vikosi vya kulinda usalama vya Somalia vimegundua pia hazina kubwa ya silaha katika maficho ya kiongozi huyo wa al Shabab.
Kwa miaka mingi sasa, nchi hiyo ya eneo la Pembe ya Afrika inasumbuliwa na mashambulizi ya kigaidi ya al Shabab ambayo yameenea pia hadi nchi jirani hususan Kenya. Mwaka 2012 kundi hilo lilitangaza rasmi kuwa ni sehemu ya mtandao wa kigaidi wa al Qaida.
Katika miaka ya huko nyuma, kundi la al Shabab lilikuwa linadhibiti maeneo mengi ya katikati na kusini mwa Somalia, hata hivyo mwaka 2015 lilipoteza maeneo mengi na hivi sasa limebakia katika baadhi ya maeneo madogo madogo tu. Hata hivyo linaendelea kufanya mashambulizi ya mara kwa mara ya kuvizia na ya kushtukiza.
chanzo:parstoday.
Comments