Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa afanya safari ya dharura nchini Somalia.


Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa leo amefanya safari ya dharura katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu, huku nchi hiyo ikiendelea kusumbuliwa na hali mbaya kutokana na uhaba wa chakula na ukosefu wa usalama.


Antonio Guterres, akitangaza safari yake hiyo katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter aliandika: Watu wapo katika hali ya kufa, ulimwengu unapaswa kuchukua hatua za kuzuia hali hii.
Mara baada ya kuwasili katika mji mkuu wa Somalia Mogadishu, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa alisema, mapigano, ukame, mabadiliko ya hali ya hewa na ugonjwa wa kipindupindu ni mambo ambayo yameifanya nchi hiyo ikabiliwe na mazingira yasiyoweza kutasawarika.
Katibu Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa, amebeba ujumbe wa amani kwa ajili ya Rais wa Jamhuri ya Somalia.
Baadaye Katibu Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa alikutana na kufanya mazungumzo na Rais mpya wa Somalia Mohamed Abdullahi Mohamed.
Rais wa Somalia amesema katika mazungumzo yake na Antonio Guterres kwamba, anayapa kipaumbele mambo na matatizo yanayoikabili nchi hiyo kama njaa na ukame akiitaka jamii ya kimataifa kuisaidia nch hiyo.
Ripoti za Umoja wa Mataifa zinaonyesha kuwa, raia milioni tano nchini Somalia wanahitaji msaada wa chakula. 
Mbali na matatizo ya ukame na njaa, Somalia imekuwa ikikabiliwa na ukosefu wa usalama na amani kutokana na mashambulio ya kundi la kigaidi la al-Shabab ambalo limewafanya wananchi wa nchi hiyo kuishi katika hali ya wasiwasi na hofu kubwa.
chanzo:parstoday.

Comments