Naibu Waziri wa
Mambo ya Ndani, Mhandisi Hamad Yusuf Masauni, ameagiza kupanguliwa kwa maofisa
wa Kitengo cha Kupambana na Dawa za Kulevya wa Idara ya Polisi na Uhamiaji
waliopo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Aman Karume mjini Unguja.
Taarifa
iliyotolewa kwa vyombo vya habari mara baada ya Masauni kutembelea uwanja huo
na Bandari kuu ya Zanzibar, ilisema kuwa baadhi ya maofisa wamekuwa na tabia ya
kuzima mashine za ukaguzi wa mizigo kwa makusudi ili kupitisha vitu haramu
zikiwamo dawa za kulevya.
“Ingawa polisi
wana kitengo maalumu cha kupambana na dawa hizi, lakini bado tatizo hili
linazidi kushamiri hapa Zanzibar,” alisema Mhandisi Masauni katika taarifa hiyo.
Pia, naibu
waziri huyo ameagiza wafanyakazi wa idara ya uhamiaji na polisi waliofanya kazi
katika eneo moja kwa zaidi ya miaka miwili kuhamishiwa kwenye vituo vingine ili
kusaidia kudhibiti uingizwaji wa dawa za kulevya visiwani humo.
Katika ziara
hiyo, Mhandisi Masauni aliambatana na Naibu Waziri wa Wizara ya Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mohamed Ahmada
Salum.
Mkuu wa idara ya
uhamiaji uwanjani hapo, Kamishna Msaidizi Fulgence Mutarasha alisema katika
vita ya kupambana na dawa hizo mwaka jana waliwakamata abiria 29 na kuwaweka
chini ya ulinzi wa Jeshi la Polisi kwa uchunguzi zaidi.
chanzo:Mwananchi.
Comments