Kampuni ya Garware yaonesha nia ya Kujenga Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano Zanzibar.


Kampuni ya Kimataifa ya Uhandisi wa  miundombinu ya Ujenzi ya Garware yenye Makao Makuu yake Mjini Bombay Nchini India imeonyesha nia yake ya kutaka kujenga Ukumbi Mpya wa Kisasa wa Kimataifa wa Mikutano Zanzibar endapo itapata fursa ya kufanya kazi hiyo.

Uwamuzi huo umekuja kufuatia Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuwa na mpango wa Kutaka kujenga Ukumbi wenye hadhi hiyo katika azma yake ya kuimarisha Sekta ya Utalii inayoonekana kuimarika na kuleta ufanisi mkubwa.

Mkurugenzi Miradi wa Kampuni Garware  Bwana Deepak Menghnani alithibitisha hilo wakati wa mazungumzo yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi mwishoni mwa ziara ya Wiki Moja ya Ujumbe wa Zanzibar hapo katika Hoteli ya Kimataifa ya Eros Mjini New Delhi India.



Bwana Deepak Menghnani alimthibitishia Balozi Seif  kwamba Wahandisi wa Kampuni ya Garware iliyoanzishwa karibu miaka sita iliyopita wana uwezo wa Kujenga Jengo la Mikutano katika kipindi kisichozidi miaka Mitatu kwa mujibu wa uwezo na mahitaji ya muhusika.

Alisema teknolojia rahisi inayotumika katika Kampuni hiyo imewawezesha Wataalamu na Wahandisi wake kuendesha ujenzi wa Majengo tofauti ikiwemo Hospitali, Skuli, Ofisi za Serikali na hata Taasisi Binafsi pamoja na nyumba za Makaazi kwa bei inayomuwezesha mtu wa kawaida kumudu kununua.

Mkurugenzi huyo wa Kampuni ya Kimataifa ya Uhandisi wa  miundombinu ya Ujenzi ya Garware alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba Taasisi hiyo ya ujenzi imekuwa ikishirikiana na Wahandisi waliobobea kutoka Nchini Misri ili kuiwezesha kuwa na uhimili wa Kimataifa.

Bwana Deepak Menghnani alisema Garware tayari imeshatoa huduma za ujenzi katika Mataifa ya Bukinafaso,Sri Lanka na Dubai ndani ya kipindi cha miaka Minane tokea kuanzishwa kwake.

Naye Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iko tayari kuwaandikia barua ya mualiko Ujumbe wa Viongozi wa Kampuni hiyo katika muda mfupi ujao ili kujionea mazingira ya Zanzibar na kuona hatua gani zinastahiki kuchukuliwa katika mwanzo wa kuelekea kwenye mpango huo wa ujenzi wa Ukumbi wa Kimataifa.

Balozi Seif alisema Zanzibar imeshafanikiwa kwa kiasi kikubwa katika uimarishaji wa Sekta ya Utalii lakini kinachokosekana kwa wakati huu ni uwepo wa Ukumbi wa Kimataifa unaotoa fursa kwa Wageni na hata Nchi rafiki kuelekeza nguvu zao za kufanya makongamano, Mikutano na hata Vikao vya Kimataifa.

“ Zipo kumbi za Mikutano zinazotumika katika baadhi ya Mahoteli Mjini na sehemu za Vijijini Zanzibar lakini hazikidhi mahitaji halisi kutokana na udogo wake ”. Alisema Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.

Balozi Seif alisema ipo mikutano na baadhi ya semina za Kimataifa zinazopangwa kufanyika Visiwani Zanzibar lakini wajumbe wa Mikutano hiyo hulazimika kuishi mbali na maeneo yao ya mikutano jambo ambalo huleta usumbufu wa kujipangia mambo yao mengine  binafsi.


Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amemaliza ziara yake Nchini India na sasa amewasili Dubai kwa Mapumziko mafupi ya siku mbili na baadae atarejea Nchini Tanzania kuendelea na majukumu yake.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
26/3/2017.

chanzo:zanzibar24.

Comments