Kamati ya Bunge yatilia shaka ujenzi DIT.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, Peter Serukamba KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii imetoa agizo kwa Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi kufanya ukaguzi wa kina katika mradi wa ujenzi wa jengo la kufundishia la Taasisi ya Teknolojia ya Dar es Salaam (DIT) na kujiridhisha kuhusu gharama na muda unaotumika katika mradi huo.

Aidha, kamati hiyo imeagiza ripoti ya ukaguzi huo ipelekwe kwao kabla ya kuanza kwa vikao vya Bajeti vya Bunge, Aprili 4, mwaka huu mjini Dodoma.


Mwenyekiti wa kamati hiyo, Peter Serukamba alitoa agizo hilo jijini Dar es Salaam baada ya kutembelea DIT ili kuona utekelezaji wa mradi wa ujenzi huo akiambatana na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Stella Manyanya.

Alisema ipo haja ya serikali kufanya ukaguzi wa kina katika mradi huo kutokana na kuchukua muda mrefu kuanzia mwaka 2008 hadi sasa bila kukamilika licha ya kubainika kuwa fedha zilikuwa zimetolewa.

“Mradi huu ulianza kwa awamu ya kwanza mwaka 2008 ukitakiwa kukamilika ndani ya mwaka mmoja, lakini baadae ukasimama, awamu ya pili ukaanza mwaka 2012 ikipangwa kukamilika mwaka 2013 kutokana na kutopata fedha kutoka serikali ulisimama na kuanza tena mwaka 2016,” alisema Serukamba.

Alisema licha ya mradi huo kukumbwa na changamoto ya kucheleweshewa fedha, lakini serikali ilipotoa fedha mwaka jana, hakukuwa na bodi iliyotakiwa kuidhinisha zabuni za ujenzi pamoja na kujua kupanda kwa gharama za ujenzi kutoka Sh bilioni 5 za awali na kufikia Sh bilioni 7 za sasa.

Aliongeza kuwa licha ya Mkuu wa DIT, Profesa Preksedis Ndomba kukiri kuwa pamoja na changamoto mbalimbali za mradi huo, lakini chuo kina fedha ambayo iko benki, lakini akashindwa kufafanua kama inaweza kukamilisha ujenzi wa jengo hilo lenye urefu wa ghorofa 10.

Alisema lengo la mradi ni kuongeza udahili wa wanafunzi wapatao 984 na ofisi za walimu 46 na limekamilika kwa asilimia 80. Naibu Waziri Manyanya aliahidi kufanyia kazi maagizo ya kamati ambayo imekuwa ikifanya jitihada ili mradi huo ukamilike.
chanzo:Habarileo.

Comments