Jumuiya za kimataifa: Yemen inaelekea kwenye maafa makubwa zaidi duniani.



Jumuiya sita za kimataifa zisizo za serikali zimejadili mashambulizi yanayoendelea kufanywa na Saudi Arabia dhidi ya watu wa Yemen kwa zaidi ya miaka miwili sasa na kutangaza kuwa, nchi hiyo iliyoathiriwa na vita inazama zaidi katika mgogoro mkubwa na wenye maafa ya binadamu.

Jumuiya sita za kimataifa zikiwemo za International Solidarity na Action Against Hunger zimetangaza katika kikao kilichofanyika jana mjini Paris,
Ufaransa kwamba mgogoro wa Yemen unaelekea kuwa moja kati ya migogoro mikubwa zaidi ya wanadamu katika dunia ya sasa.

Taarifa iliyotolewa na jumuiya hizo imesema jumuiya za misaada ya kibinadamu zinakabiliwa na matatizo makubwa nchini Yemen kuliko eneo lolote jingine duniani.

Hivi karibuni pia taarifa ya Umoja wa Mataifa ilisema kuwa, njaa, vizingiti vya aina mbalimbali na kuzuiwa operesheni za misaada ya kibinadamu kupelekwa kwa waathirika, na mashambulizi yanayoendelea kufanywa na Saudi Arabia na washirika wake dhidi ya watu wa Yemen vimeitumbukiza nchi hiyo katika mgogoro mkubwa. 

Taarifa hiyo imesema kuwa watu milioni 26 ambao hata kabla ya kuanza vita nchini Yemen walikuwa wakikabiliwa na umaskini, sasa wanasumbuliwa na hali mbaya zaidi.

Taarifa ya Umoja wa Mataifa inasema zaidi ya nusu ya hospitali na vituo vya afya nchini Yemen vimeharibiwa kwa mashambulizi ya Saudi Arabia na kwamba raia wa kawaida wanasumbuliwa na maradhi ya aina mbalimbali yakiwemo ya kipindupindu na utapiamlo.

Saudi Arabia inaizingira Yemen kutoka pande zote za anga, nchi kavu na baharini na inazuia kuingizwa misaada ya kibinadamu nchini humo.

Dominik Stillhart, Mkurugenzi wa Operesheni za Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu ametahadharisha kuwa, iwapo hatua za dharura hazitachukuliwa mamilioni ya raia wa Yemen watapoteza maisha kutokana na njaa.
chanzo: parstoday.

Comments