Serikali ya Gambia imetangaza kuwa itaunda tume ya ukweli na maridhiano
na kuwalipa fidia waathirika wa jinai zilizofanywa na serikali ya
aliyekuwa rais wa nchi hiyo Yahya Jammeh inayotuhumiwa kuwatesa na
kuwaua watu walioshukiwa kuwa wapinzani wa serikali hiyo.
Waziri wa
Sheria wa Gambia Abubacarr Tambadou
amesema kupitia taarifa kuwa
serikali itachunguza pia fedha za Jammeh aliyekimbilia uhamishoni Guinea
ya Ikweta mwezi Januari baada ya kufikia kikomo utawala wake ulioanzia
mwaka 1994 alipotwaa madaraka kupitia mapinduzi ya kijeshi.
Tambadou
amefafanua kuwa tume hiyo ya ukweli na maridhiano itakayozingatia pia
kuwalipa fidia waathirika itaundwa katika kipindi cha miezi sita ijayo
na vikao vya kupokea na kusikiliza maoni ya wananchi vinategemewa kuanza
mwishoni mwa mwaka huu.
Tangu serikali mpya ya Rais Adama Barrow iingie madarakani nchini
Gambia imechukua hatua kadhaa za kurejesha utawala wa sheria na
kuimarisha vyombo vya mahakama.
Serikali
ya Banjul inakusudia kutafiti kwanza tume za aina hiyo zilizoundwa
katika mataifa mengine.
Itakumbukwa kuwa Afrika Kusini iliunda Tume ya
Ukweli na Maridhiano baada ya kutokomezwa mfumo wa utawala wa ubaguzi wa
rangi wa Apatheidi nchini humo; hatua ambayo iliingwa na mataifa
mengine kadhaa ya Kiafrika.
chanzo: parstoday.
Comments