Idadi ya mabilionea (wa dola) duniani imeongezeka kwa asilimia 13 na kufikia 2, 043.
Kwa mujibu wa jarida hilo, mali ya Bw Gates imeongezeka hadi $86bn, kutoka $75bn.
Anafuatwa na Warren Buffett, aliyeongeza utajiri wake kwa $14.8bn hadi $75.6bn.
Rais
wa Marekani Donald Trump, hata hivyoa meshuka nafasi 220 hadi 544
kwenye orodha hiyo ya matajiri na sasa ana mali ya $3.5bn pekee.
Forbes
wamesema kushuka kwa utajiri wa Bw Trump kwa $1bn kulitokana na
kuupungua kwa kasi ya sekta ya biashara ya ardhi na makao Marekani.
Katika orodha hiyo ya Forbes, mabilionea 183 walijipatia utajiri
wao kupitia teknolojia, utajiri wao ukiwa jumla ya dola trilioni moja
za Marekani.
Orodha hiyo imetawaliwa na mabilionea kutoka Marekani.
Wengine
walio kwenye 10 matajiri zaidi ni mwanzilishi wa Amazon Jeff Bezos,
ambaye amepanda hadi nambari tatu utajiri wake ukiongezeka kwa kiwango
cha juu zaidi kuliko wa mtu mwingine yeyote duniani.
Utajiri wake uliongezeka kwa $27.6bn hadi $72.8bn.
Mwanzilishi wa Facebook Mark Zuckerberg yupo nafasi ya tano na mwanzilishi mwenza wa Oracle Larry Ellison alikuwa nambari saba.
Idadi ya mabilionea duniani ambao sasa wanafikia 2,043, ilipata
ongezeko kubwa zaidi kwa mwaka mmoja katika kipindi cha miaka 31 tangu
orodha hiyo ianze kuandaliwa.
Mabilionea kutoka Marekani walikuwa
565, jambo ambalo Forbes wanasema huenda lilitokana na kuimarika kwa
soko la hisa pakubwa tangu Trump aliposhinda uchaguzi Novemba 2016.
China ilikuwa ya pili kwa mabilionea ikiwa na mabilionea 319 nayo Ujerumani ya tatu na mabilionea 114.
Watu 10 matajiri zaidi:
- Bill Gates (mwanzilishi mwenza wa Microsoft): $86bn
- Warren Buffett (mwekezaji Mmarekani): $75.6bn
- Jeff Bezos (mwanzilishi wa Amazon): $72.8bn
- Amancio Ortega (mwanzilishi wa Inditex): $71.3bn
- Mark Zuckerberg (mwanzilishi wa Facebook): $56bn
- Carlos Slim (mfanyabiashara kutoka Mexico): $54.5bn
- Larry Ellison (mwanilishi mwenza wa Oracle): $52.2bn
- Charles Koch (mfanyabiashara Mmarekani): $48.3bn
- David Koch (mfanyabiashara Mmarekani): $48.3bn
- Michael Bloomberg (mwanzilishi wa Bloomberg): $47.5bn
Wanawake katika orodha hiyo waliongezeka hadi 227 kutoka 202, na wanamiliki jumla ya $852.8bn.
Kwa
mwaka wa pili, Mfaransa Liliane Bettencourt, wa maduka ya bidhaa za
urembo L'Oreal, alikuwa mwanamke tajiri zaidi duniani akiwa na mali ya
$39.5bn. Alirithi biashara hiyo.
Wengi wa wanawake matajiri duniani walirithi utajiri wao, Forbes walisema.
Lakini pia wapo wafanyabiashara 15 wa kike ambao hawakurithi mali, sana kutoka Asia.
Mmoja ni Nguyen Thi Phuong Thao kutoka Vietnam anayemiliki kampuni ya safari za ndege ya VietJet.
Kuyumba kwa Trump
Forbes
wanasema utajiri wa Rais wa Marekani Donald Trump ulishuka kutokana na
kupungua kasi kwa ukuaji wa soko la ardhi na nyumba Manhattan, ambapo
utajiri wake mwingi upo.
"Asilimia arobaini ya utajiri wa Donald Trump upo
Trump Tower na katika majumba mengine manane yanayopatikana eneo la nusu
kipenyo cha maili moja," Forbes walisema.
"Hivi karibuni, eneo hilo limetatizika kibiashara."
Jarida
hilo pia limesema utajiri wake uliathiriwa pia na matumizi katika
siasa, sana kwenye kampeni yake ya urais ambapo inakaribiwa alitumia
$66m.
Aidha, alitumia $25m kumaliza kesi ambapo alishtakiwa kwa tuhuma za kuwatapeli wanafunzi kupitia Chuo Kikuu cha Trump.
chanzo:Bbc.
Comments