
Dkt. Shein aliyasema hayo katika mkutano wake na waandishi wa habari
katika uwanja wa ndege wa Zanzibar mara baada ya kurejea kutoka
Indonesia ambapo alisema kuwa deni hilo la TANESCO limekuwepo kwa miaka
mingi na kwamba si la jana wala leo, hivyo kama umeme utakatwa wao
watatumia vibatari.
“Tungoje basi uzimwe kama nyie muna wasiwasi, mimi najua hawezi
kuuzima, kwa sababu deni hatujaanza kudaiwa leo sisi. Miaka 20 imepita
tunadaiwa, kwahiyo mimi sitaki niseme sana leo kwenye hili na kama
watazima basi, tutawasha vibatari vyetu, hatuna tatizo sisi. Lakini
sidhani Tanzania iliyomakini kama inaweza kufanya vitu kama hivyo na
sina uhakika kama magazeti yameandika vizuri,” alisema Dkt. Shein.
Aidha, Dkt Shein alisema haamini kama umeme utakatwa na kwamba
pengine waandishi wa habari ndio waliokosea kuandika habari hiyo, lakini
alisema yeye kama Rais wa Zanzibar atahakikisha deni hilo linalipwa.
TANESCO ilitoa siku 14 kwa wateja wake wote linalowadai kulipa madeni
yao, vinginevyo litasitisha utoaji wa Huduma ya Nishati kwa wahusika.
Akifafanua zaidi Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Dkt. Tito
Mwinuka alisema, Wizara na Taasisi za Serikali zinadaiwa zaidi ya
Shilingi Bilioni 52.53, Shirika la Umeme Zanzibar, (ZECO), linadaiwa
zaidi ya Shilingi Bilioni 127.87, na Makampuni binafsi na Wateja wadogo
wadogo deni ni zaidi ya Shilingi Bilioni 94.97.
chanzo: zanzibar24.
Comments