Dk. Shein afanya mazungumzo na Wataalamu wa upasuaji wa kichwa na uti wa mgongo.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameeleza kuwa idadi kubwa ya wagonjwa waliofanyia upusuaji wa maradhi ya kichwa na uti wa mgongo hapa Zanzibar tokea kuanzishwa huduma hizo ni miongoni mwa mafanikio makubwa katika sekta ya afya hapa nchini.
Dk. Shein aliyasema hayo leo wakati alipokuwa na mazungumzo na ujumbe wa Wataalamu wa upasuaji wa kichwa na uti wa mgongo waliofika Ikulu mjini Zanzibar.

Wataalamu hao ambao  wapo Zanzibar kushiriki mkutano maalum wa mafunzo kuazia kesho tarehe 28 hadi  tarehe 30 mwezi huu ambapo pia, ni miongoni mwa maadhimisho ya kutimiza miaka miwili tokea kuaizishwa kwa jengo la huduma hizo katika hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja mjini Zanzibar, ambalo alilizindua Dk. Shein Januari 9, kwaka 2015.
Katika maelezo yake Dk. Shein alisema kuwa mafanikio hayo yanatokana na juhudi kubwa zinazochukuliwa na wataalamu wa fani hiyo kutoka sehemu mbali mbali duniani ambao wanaiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta ya afya hasa katika kutoa huduma ya upasuaji huo.
Dk. Shein alisema kuwa hatua za utoaji wa huduma hiyo zinazofanywa kwa Unguja na Pemba ambazo tayari zaidi ya wagonjwa 500 wameshafanyiwa upasuaji huo wakiwemo watoto, wanawake na watu wazima zimeweza kusaidia kwa kiasi kikubwa kuimarisha sekta ya afya hapa nchini.
Alieleza kuwa kuwepo kwa wagonjwa mbali mbali wanaotoka nje ya Zanzibar na kuja kupata huduma hiyo hapa Zanzibar ni historia ambayo inajirejea ambayo ilikuwepo hapa Zanzibar tokea wakati wa ukoloni ambapo wagonjwa mbali mbali kutoka nje ya Zanzibar walikuja kupata huduma za afya hapa nchini.
Alisema kuwa licha ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuokoa kiasi kikubwa cha fedha zilizokuwa zikitumika kwa ajili ya kuwatibu wagonjwa wa maradhi hayo nje ya nchi faraja iliopo ni kuona huduma hiyo muhimu inatolewa hapa nchini na kuweza kuwasaidia wananchi mbali mbali wa ndani na nje ya Zanzibar.
Aidha, Dk. Shein aliueleza ujumbe huo juhudi zilizochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuhakikisha inanunua vifaa muhimu na vya kisasa  ikiwemo mashine ya “MRI”, mashine ya “X-ray” pamoja na mashine za huduma za kusafisha damu kwa wagonjwa wenye matatizo ya figo, ambazo zote hizo zimeshanunuliwa na serikali na kuanza kutoa huduma kwa wananchi.
Mbali ya juhudi hizo, Dk. Shein aliueleza ujumbe huoa azma ya Serikali ya kujenga hospitali mpya ya mafunzo ambayo  mbali na mambo mengine pia, itatoa mafunzo juu ya upasuaji wa kichwa na uti wa mgongo, azma ambayo iliungwa mkono na mkuu wa Kanda wa Hospitali za Aga Khan, Shawn Balouki ambaye ni miongoni mwa wajumbe waliofika Ikulu.
Nao Wataalamu hao wakiongozwa na Rais wa Taasisi ya Maendeleo ya Elimu inayohusiana na upasuajai wa Mishipa ya Fahamu, Uti wa mgongo na Vichwa maji (NED), Dk. Hosea Piquer pamoja na Dk. Mahmood Quiresh walieleza mafanikio makubwa waliyoyapata katika huduma za upasuajai walizozifanya tokea kuanzishwa huduma hizo hapa nchini.
Katika maelezo yao wataalamu hao walimuhakikishia Dk. Shein kuwa wataendelea kuziunga mkono juhudi zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha sekta ya afya hasa katika  huduma hiyo ya upasuaji wa kichwa na uti wa mgongo.
Sambamba na hayo, Wataalamu hao walitumia fursa hiyo kumueleza Dk. Shein azma ya kuendelea na utoaji huduma hizo Unguja na Pemba pamoja na mkutano maalum wa mafunzo wa siku tatu kuzia kesho (tarehe 28-30, 2017) katika Taasisi ya maradhi hayo iliyopo katika Hospitali ya Mnazi Mmoja mjini Zanzibar.
Wataalamu hao walieleza kuwa mbali ya kuwafanyia upasuaji wagonjwa wa Zanzibar tayari wameshawafanyia upasuaji wagonjwa kutoka Lamu, Dubai na sehemu nyengine nje ya Zanzibar jambo ambalo ni mafanikio huku wakieleza kupokea wataalamu kutoka nchi mbali mbali za bara la Afrika wanaokuja kujifunza namna ya kuanzisha na kuendeleza taasisi kama hiyo.
Taasisi kama hiyo ni ya pekee katika bara la Afrika ambayo inatoa huduma hizo bure pamoja na kutumia vifaa vya kisasa na utaalamu na wataalamu wakubwa kutoka sehemu mbali mbali duniani wakiwemo kutoka nchini Spain, Ujerumani, Pakistan, Aga Khan na sehemu nyenginezo.
Pamoja na hayo, wataalamu hato walieleza namna wanavyochukua juhudi za kutoa mafunzo wa wataalamu wazalendo huku wakieleza mashirikiano mazuri wanayoyapata kutoka kwa wataalamu wazalendo.
Katika mazungumzo hayo ambapo Madaktari hao bingwa walikuwa wameongozana na uongozi wa Wizara ya Afya chini ya Waziri wa Wizara hiyo  Mahmoud Thabit Kombo, ambao walipongeza mashirikiano makubwa wanayoyapata katika kutekeleza shughuli zao hapa nchini.
Pamoja na hayo, madaktari hao walieleza kuwa miongoni mwa mafanikio makubwa yaliopatikana kutoka kwa Taasisi hiyo ni pamoja na kufanya upasuaji huo kwa wagonjwa zaidi ya 500 wakiwemo watoto, wanawake na watu wazima na kueleza jinsi Serikali ilivyokuw ikitumia fedha nyingi kuwapelekea wagionjwa wa maradhi hayo nje ya nchi kabla ya kuanzishwa kwa huduma hizo hapa nchini.
Madaktari hao walimueleza Dk. Shein kuwa gharama hizo ni kwa ajili ya taaluma na upasuaji mbali na gharama nyengine ambazo Serikali ingeweza kutumia katika usafirishaji, gharama za malazi na chakula kwa wagonjwa na wauguzi wao pale wanapowasafirisha kwenda nje ya nchi.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar.
chanzo:zanzibar24.

Comments