Wagombea wote waliochukua fomu kutoka vituo vya Dodoma, Zanzibar na
Dar es Salaam wanatakiwa kuripoti Ofisi Ndogo ya CCM Lumumba Dar es
Salaam
keshokutwa saa 3.00 asubuhi wakiwa na vyeti vyao vya taaluma
pamoja na hati ya kusafiria au kadi ya kupigia kura.
Wakizungumza na gazeti hili, wagombea waliofika kuchukua fomu
kutafuta tiketi ya kugombea nafasi tisa za kuingia kwenye Bunge la
Afrika Mashariki, walisema wanatakiwa kufika katika ofisi hiyo wakiwa na
vyeti vyao vya taaluma.
Wagombea hao wanatakiwa kuwapo ofisini hapo siku moja baada ya kujaza
fomu na na kuzirudisha na kwamba siku ya mwisho ya kurudisha ni kesho
saa 10.00 jioni.
Akizungumza mjini hapa baada ya kuchukua fomu, mgombea Watson
Mwakwalila (31) ambaye ni mtaalamu wa masuala ya upimaji wa ardhi,
alisema anaingia katika kinyang’anyiro cha kutafuta nafasi moja kati ya
tisa za ubunge wa Afrika Mashariki ili akatetee na kupigania masuala ya
ardhi.
“Nataka kuacha historia kwamba mgombea aliyewahi kugombea uspika wa
Bunge la Jamhuri ya Muungano, amepigania masuala ya ardhi katika Bunge
la Afrika Mashariki,” alisema Mwakwalila.
Mgombea mwingine, Pius Lufutu (28) aliywakuwa wa 55 kuchukua fomu
katika kituo cha Dodoma, na akiwa ni mtaalamu wa masuala ya Uhusiano wa
Umma na Masoko, amesema anataka kuwa mbunge wa EALA ili kupigania
ushindani wa bidhaa katika soko la Afrika Mashariki.
“Nataka kuingia nafasi hiyo kwanza kutoa woga ambao vijana wengi wa
Tanzania wanao, kwa kupigania soko la mazao kwa vijana na akinamama
ambao ni wajasiriamali wengi,” alisema Lufutu na kuongeza kuwa, vijana
wengi wamejitokeza ili kuingia bungeni kutetea maslahi ya vijana na pia
lugha ya Kiswahili ambayo ni lugha ya Afrika Mashariki.
Kitendo cha CCM kuwataka makada wake waende na vyeti, kinalenga kuchagua wenye sifa za kweli kuwania ubunge huo.
Watahakikiwa vyeti kuanzia keshokutwa saa 3 asubuhi na baada ya
kuhakikiwa, wenye vyeti bandia wataondolewa na wengine wataingia
kuhojiwa kwenye KamatiKuu (CC) ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) na
wachache watafikishwa mbele ya Bunge la Jamhuri ili kupigiwa kura na
kubaki tisa tu kuwa wabunge wa wakilishi kutoka Tanzania kwenye Bunge
hilo.
Bunge la Afrika Mashariki ni chombo cha Jumuiya ya Afrika Masharki
kilichoanzishwa chini ya Ibara ya 9 ya Mkataba wa Uanzishaji Jumuiya
hiyo na kwa sasa lina nchi tano wanachama ambazo ni Kenya, Tanzania,
Uganda, Rwanda, Burundi na Sudan Kusini kila nchi inatakiwa kutoa
wabunge tisa kwa ajili ya kuunda bunge hilo.
chanzo:Habarileo.
Comments