Taarifa ya Duwasa kwa kamati hiyo ilipotembelea miradi ya mamlaka
hiyo juzi mjini hapa, inaonesha kuwa mamlaka hiyo imeboresha huduma za
upatikanaji wa maji kutoka wastani wa saa 16 kwa siku hadi saa 22.
Kamati imetaka yapatikane kwa saa 24.
Aidha, mamlaka hiyo imetakiwa pia kutekeleza agizo la Rais John
Magufuli kwa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kuwakatia umeme wadaiwa
sugu, kwa wao (Duwasa) kuzikatia maji taasisi zote wadaiwa sugu
zikiwemo za serikali.
“Sasa serikali inahamia Dodoma, maji yanatakiwa kupatikana kwa saa 24
na si 22 tena,” alisema mjumbe wa kamati hiyo, Mbunge wa Tanga Mjini,
Mussa Mbarouk (CUF).
Mbarouk aliipongeza Serikali ya Awamu ya Nne chini ya uongozi wa Rais
Jakaya Kikwete kwa kuhakikisha huduma ya maji inaboreka mkoani Dodoma
ingawa yapo maeneo bado katika mkoa huo yanahitaji nguvu ya ziada.
“Sasa hata msikitini maji yanapatikana, namuomba Mwenyezi Mungu
amlipe JK (Rais mstaafu Jakaya Kikwete) kwa hili,” alisema Mbarouk na
kutoa dua hiyo kwa Rais mstaafu Kikwete.
Naye Mbunge wa Viti Maalumu, Yosefa Komba (Chadema) aliitaka Duwasa
kuhakikisha mji wa Dodoma unapata maji katika kata zote na maeneo ya
pembezoni kwa kuwa mkoa unatanuka kutokana na serikali kuhamia huko.
Kuhusu kuzikatia maji taasisi zilizo wadaiwa sugu, Mbarouk alisema
agizo la Rais Magufuli alilolitoa kwa Tanesco, lihamie katika maji.
Mkurugenzi wa Duwasa, David Pallangyo alisema mamlaka inapokea ushauri
wa kamati na itachukua hatua.
chanzo:Habarileo.
Comments