Bodaboda haziruhusiwi kubeba abiria Zanzibar.

WIZARA ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imesema usafiri wa vyombo vinavyotumia magurudumu mawili, ikiwemo bodaboda havijaruhusiwa kutoa huduma za usafiri kwa abiria Zanzibar.
Kaimu Waziri wa Ujenzi Mawasiliano na Usafirishaji, Issa Haji Usi Gavu ametoa msimamo huo wakati anajibu swali la Mwakilishi wa Jimbo la Jangombe, Abdalla Maulid Diwani aliyetaka kufahamu vijana wanaotoa huduma za usafiri bodaboda kwa nini hadi sasa hawajapatiwa kibali cha kutoa huduma hizo kwa mujibu wa sheria.

Gavu amesema, kwa mujibu wa sheria za usafiri wa vyombo vya magurudumu mawili ni marufuku kufanya kazi za kutoa huduma za usafiri kwa abiria.
Hata hivyo, alisema serikali inathamini kazi za kutoa huduma zinazofanywa na vyombo hivyo kwa hivyo imeridhia kufanya kazi za kubeba abiria huku taratibu nyingine zikitayarishwa.
“Mheshimiwa Spika nataka kuwajulisha wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kwamba kwa mujibu wa sheria ya kutoa huduma za usafiri wa abiria kwa vyombo vya magurudumu mawili ni marufuku kubeba abiria kwa sasa ingawa serikali inatambua kufanya kazi kwa vyombo hivyo,” amesema.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, Wizara ya Mawasiliano kwa kushirikiana na Serikali za Mitaa inatarajiwa kuweka miongozo na masharti bora zaidi ambayo yatasaidia kuwepo kwa utaratibu mzuri wa kutoa huduma kwa vyombo hivyo.
Amesema serikali imeridhishwa kwa kiasi kikubwa kwa kazi ya kutoa huduma za usafiri kwa vyombo vya abiria vya magurudumu mawili ambapo ajira kwa vijana imeimarishwa.
Kwa mfano, alisema usafiri wa bodaboda umesaidia kuwafikisha abiria zaidi katika maeneo ya ndani katika nyakati tofauti ikiwemo usiku ambapo hakuna matukio ya uhalifu dhidi yao yaliyoripotiwa hadi sasa.
“Serikali imeridhika na kazi nzuri inayofanywa na madereva wa Bodaboda katika kutoa huduma za usafiri kwa wananchi ambapo tupo katika hatua za mwisho za kuweka utaratibu mzuri wa usafiri,” amesema.
chanz:habarileo.

Comments