
Balozi Seif anaeondoka na Mkewe Mama Asha Suleiman Iddi akiuongoza Ujumbe wa Viongozi Wawili pamoja na Makatibu Wakuu wa Wawili wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Viongozi hao ni Mjumbe wa Baraza la Mapinduzi ambae pia ni Waziri asiye na Wizara Maalum Dr. Sira Ubwa Mamboya, Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Mihayo Juma N’hunga, Katibu Mkuu Wizara ya Afya Bibi Asha Ali Abdulla na Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi Nd. Ali Juma Ali Juma.
Balozi Seif na Ujumbe wake ataanza ziara yake Tarehe 20 Machi kwa kutatembelea maeneo ya Kilimo ikiwemo mashamba ya Viungo, Viwanda na Viunganishi vyake pamoja na kukagua masoko ya mazao ya Kilimo katika Jimbo la Kerala.
Tarehe 21 na 22 Machi, Ziara ya Balozi Seif itawaunganisha kwa kuzitembelea Hospitali Maarufu Nchini India za Chenai, Apolo na Bangalore ambazo atapata fursa ya kukagua baadhi ya wagonjwa wa Tanzania wanaopata huduma za Afya kwenye Hospitali hizo.
Pamoja na mambo mengine Ujumbe huo utafanya mazungumzo na Uongozi wa Hospitali hizo ambapo baadaye watasaini Mkataba wa maeneo ya mashirikiano katika sekta za Afya baina ya Uongozi wa Hospitali hizo na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Mjini New Delhi Ujumbe wa Balozi Seif utatembelea Kiwanda cha Matrekta cha Mahendra ambacho tayari kimeshatiliana saini na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mkataba wa Kuleta Matrekta kwa ajili ya kuendeleza Kilimo Visiwani Zanzibar.
Baadae Ujumbe huo wa Zanzibar utazuru Taj Mahal, kuangalia Teknolojia ya Kisasa ya Umwagiliaji itakayokwenda sambamba na mazungumzo ya kuimarisha uhusiano kati ya Uongozi wa Taasisi hizo na Ujumbe huo wa Zanzibar.
Ziara ya Ujumbe huo wa Zanzibar itatoa nafasi ya kukutana kwa mazungumzo na Wafanyabiashara pamoja na Wawekezaji wa Nchini India kuwaelezea azma ya Zanzibar ya kufungua milango ya uwekezaji hasa katika Sekta za Utalii, Kilimo, Afya na Mawasiliano.
Balozi Seif atamaliza ziara yake Nchini India mnamo Tarehe 25 Machi kwa kufanya uchunguzi wa kawaida wa Afya yake na usiku ataondoka Nchini humo kupitia Dubai kwa mapumziko mafupi na baadaye kurejea Zanzibar Tarehe 28 Machi mwaka 2017.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
17/3/2017.
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
17/3/2017.
chanzo: zanzibar24.
Comments