
Alisema suala la nidhamu ambalo ndilo kigezo pekee kilichopelekea Umoja wa Mataifa kuyaamini Majeshi
ya Tanzania katika ulinzi wa amani katika Nchi zenye migogoro ya vita vya wenyewe kwa wenyewe hasa Barani Afrika linapaswa kusimamiwa kwa nguvu zote.
Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo wakati akizungumza na Mkuu Mpya wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama Tanzania Generali Venance Mabeyo aliyeteuliwa hivi karibuni na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. John Pombe Magufuli ambae alifika kujitambulisha rasmi Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Alisema umahiri wa Majeshi hayo katika ulinzi wa Kimataifa,Kitaifa, Raia, pamoja na Mali zao umepelekea kuaminika vyema kitendo ambacho kimewapa faraja Wananchi walio wengi hapa Nchini pamoja na Mataifa wanayopangiwa kusimamia Ulinzi wa Amani.
Hata hivyo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema zipo baadhi ya changamoto zinazoyakabili Majeshi hayo ya Ulinzi na Usalama Nchini, lakini umahiri uliopo wa Viongozi na Maafisa wa Vikosi hivyo changamoto hizo zitapungua au kuondoka kabisa.

Balozi Seif aliwashauri Wananchi kujiepusha na tabia ya kuyatumia maeneo yaliyo karibu na Kambi za ulinzi kwa kujenga nyumba za makaazi ya kudumu au kulima ili kujikinga na hitilafu zinazoweza kutokea za miripuko ya silaha nzito ambazo baadae huleta athari za kiafya au wakati mwengine vifo.
Mapema Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama Tanzania Generali Venance Mabeyo alimuhakikishia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba majeshi ya Ulinzi na Usalama ya Tanzania yataendelea kuwajali na kuwaheshimu Wananchi kwani wao ni sehemu ya Majeshi hayo.
General Mabeyo alisema vijana wanaounda Majeshi hayo ya Ulinzi ni miongoni mwa Watoto, ndugu na Jamaa wa damu wa Wananchi wa Taifa hili wanaohitaji kuendelea kupewa ushirikiano utakaodumisha upendo na mshikamano wa pande mbili husika.
Mkuu huyo wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama Tanzania amezishukuru Serikali zote mbili za Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na ile ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuyawezesha Majeshi hayo kutekeleza vyema majukumu yao ya ulinzi ya kila siku.
Alieleza kwamba Majeshi hayo yako tayari kuendelea kupokea maagizo, ushauri na hata msaada kutoka kwa Viongozi wa Kitaifa na Wananchi na Raia wema katika kuona usalama na amani wa Taifa la Tanzania unaendelea kushamiri wakati wote.

chanzo:zanzibar24..
Comments