Al-Sisi: Misri inapongeza juhudi za jeshi la Syria katika kuwatokomeza magaidi.

Rais Abdel Fattah el-Sisi wa Misri amesema kuwa, sambamba na nchi yake kufungamana na misingi ya kutoingilia masuala ya ndani ya Syria, pia inaunga mkono juhudi za jeshi la nchi hiyo katika kuwatokomeza magaidi.

Rais el-Sisi ameyasema hayo mjini Cairo, katika mkutano wa pamoja wa waandishi wa habari akiwa na Kansela wa Ujerumani Bi, Angela Merkel na kuongeza kuwa, nchi za eneo la Mashariki ya Kati zinazounga mkono magaidi, zinatakiwa kukomesha mwenendo huo. 


Akisisitizia udharura wa kulindwa umoja wa ardhi ya Syria na kuharakishwa ukarabati wa nchi hiyo, amezitaka nchi waungaji mkono wa ugaidi kuacha hatua zao hizo.

Kadhalika Rais Abdel Fattah el-Sisi amesema kuwa kuimarishwa usalama nchini Libya, ni suala ambalo litasaidia kudumisha usalama na amani katika eneo na hata Ulaya na kusisitiza kwamba, sasa umefika wakati kwa nchi waungaji mkono wa ugaidi kufungamana na suala hilo. 
Kwa upande wake, Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel amesema kuwa, kamwe mgogoro wa Syria hauwezi kutatuliwa kwa njia ya kijeshi na badala yake unatakiwa kutatuliwa kwa njia za kisiasa chini ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa.

Safari ya Bi, Merkel nchini Misri pia ilikuwa na lengo la kuishawishi Cairo kuungana na mpango wa kupambana na wahajiri haramu kuelekea barani Ulaya. Hii ni katika hali ambayo kabla ya Kansela wa Ujerumani kufanya safari hiyo nchini Misri, Shirika la Msamaha Duniani (Amnesty International)  lilikuwa limemtaka Bi, Merkel kuzungumza na Rais el-Sisi kuhusiana na faili la ukandamizaji wa haki za binaadamu nchini Misri. 

Itakumbukwa kuwa baada ya kuondolewa madarakani rais aliyechaguliwa na wananchi Muhammad Mursi na kuingia madarakani Abdel Fattah el-Sisi, nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika ilishuhudia machafuko makubwa yaliyoandamana na ukandamizaji wa kutisha dhidi ya wapinzani wa serikali ya sasa.
chanzo:parstoday.

Comments