
Dk. Shein aliyasema hayo leo, Ikulu mjini Zanzibar wakati alipofanya mazungumzo
na Ujumbe wa Wakurugenzi Watendaji wa Benki ya Maendeleo ya Afrika AfDB wanaofanyakazi zao ndani na nje ya Bara la Afrika, ujumbe ulioongozwa na Bi Lekhethe Mmakgoshi kutoka Afrika Kusini, anaeiwakilisha Afrika Kusini, Swaziland na Lesotho.
Katika mazungumzo hayo, Dk. Shein alieleza kuwa ujio wa viongozi hao wakuu 12 kutoka AfDB kuja Zanzibar umeonesha wazi jinsi Benki hiyo inavyoithamini Zanzibar na kujali juhudi zake katika kuimarisha miradi ya maendeleo iliyo chini ya benki hiyo sambamba na kuimarisha uhusiano na ushirikiano uliopo.
Dk. Shein alisema kuwa AfDB imeweza kuunga mkono juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha miradi mbali mbali ya maendeleo hasa katika sekta ya miundombinu ya barabara kwa upande wa Unguja na Pemba.
Akieleza juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha uchumi na kuimarisha sekta za maendeleo, Dk. Shein aliwaeleza viongozi hao azma ya Serikali ya kuujenga upya uwanja wa ndege wa Pemba ili uweze kutoa huduma sawa na uwanja wa ndege wa Abeid Amani Karume uliopo Unguja na kuongeza kuwa tayari upembuzi yakinifu umeshafanywa na hivi sasa mchakato katika azma hiyo unaendelea.
Dk. Shein aliongeza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imechukua juhudi kubwa katika kuutengeneza uwanja wa ndege wa Abeid Amani Karume kwa kuzipanua njia za kurukia na kutulia ndege katika uwanja huo pamoja na ujenzi wa jengo jipya la abiria katika kiwanja hicho ambapo kumaliza kwake kutaongeza idadi ya watalii wanaoingia nchini.
Aidha, Dk. Shein aliipongeza AfDB kwa azma yake ya kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika miradi mengine mipya ya maendeleo sambamba na kuiendeleza ile ya iliyopo hatua ambayo alisema itazidi kuimarisha uchumi na kukuza sekta nyengine za kijamii na kimaendeleo.
Dk. Shein aliongeza kuwa AfDB imesaidia kwa kiasi kikubwa kusaidia juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha sekta ya afya juhudi ambazo zimechangia kupunguza vifo vya akina mama na watoto.
Sambamba na hayo, Dk. Shein alitumia fursa hiyo kuueleza ujumbe huo kuwa Zanzibar ni miongoni mwa nchi za Bara la Afrika zinazopokea watalii wengi kutokana na mazingira na vivutio mbali mbali vilivyopo.
Hivyo, Dk. Shein aliwakaribisha viongozi hao kuja kuitembela Zanzibar wakati wa mapumziko yao.
Nao ujumbe huo wa Wakurugenzi Watendaji wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) ulimuhakikishia Dk. Shein kuwa Benki hiyo itaendelea kuiunga mkono Zanzibar na kupongeza juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuwaletea maendeleo wananchi wake.
Akizungumza kwa niaba ya ujumbe huo Mkurugenzi Mtendaji wa AfDB anayeziwakilisha nchi za Afrika ya Kusini, Lesotho na Swaziland Bi Lekhethe Mmakgoshi alieleza kuwa ujio wao Zanzibar ni kuja kujionea juhudi zinazochukuliwa katika kuimarisha miradi ya maendeleo iliyo chini ya Benki hiyo sambamba na kuchukua vipaombele vilivyowekwa katika kuendeleza miradi hiyo.
Aidha, Bi Mmakgoshi alieleza kuwa ujumbe huo umefarajika kwa kiasi kikubwa na hatua za kuendeleza miradi ya maendeleo ya Benki hiyo inayotekelezwa hapa Zanzibar na kuahidi azma ya Benki hiyo ya kuanzisha miradi mengine mipya na kuedneleza ile iliyopo ambayo inaendelea ikiwemo ile ya barabara.
Sambamba na hayo, kiongozi huyo wa AfDB alimueleza Dk. Shein kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwemo Zanzibar imekuwa na utaratibu mzuri katika utekelezaji wa miradi iliyo chini ya Benki hiyo juhudi ambazo zinafaa kuungwa mkono.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar.
chanzo:zanzibar24.
Comments