
Alisema Oman imejitolea kwa nguvu zake kuunga mkono harakati za
maendeleo na uchumi za Zanzibar kupitia udumishwaji wa ushirikiano huo
ulioasisiwa na Viongozi wakuu wa pande hizo mbili.
Balozi Seif Ali Iddi alieleza hayo wakati akibadilishana mawazo na
Balozi Mdogo Mpya wa Omar aliyepo Zanzibar Dr. Ahmed Humoud Al – Habsi
aliyefika kujitambulisha rasmi Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Alishauri ziara za kukuza ushirikiano wa pande hizo mbili kwa
kujumuisha Maafisa wa Taasisi, mashirika na hata jumuiya za kiraia
uendelee kuimarishwa zaidi badala ya kuziachia ziara za sehemu hizo
kufanywa na Viongozi wakuu pekee.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliipongeza Serikali ya Oman chini
ya Utawala wa Mfalme Qabous Bin Said kwa misaada mbali mbali ya
maendeleo inayotowa kwa Zanzibar.
Balozi Seif aliutolea mfano msaada mkubwa wa Kiwanda cha Uchapaji
Maruhubi kilichopata msukumo wa vifaa vya kisasa vilivyogharamiwa na
Serikali ya Oman ambao ni hazina kubwa kwa Zanzibar.
Alisema miundombinu ya kisasa ya vifaa vilivyofungwa kwenye Kiwanda
hicho cha Uchapaji itawezesha kazi zote za Serikali, Taasisi na
Mashirika yake hivi sasa kuchapishwa katika kiwanda hicho.
Akigusia suala la Mafuta na Gesi Asilia Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar alimuomba Balozi huyo Mdogowa Oman aliyepo Zanzibar Dr. Ahmed
kuyashawishi Makampuni ya Nchi yake kufikiria wazo la Zanzibar katika
kutaka kuwekeza kwenye Sekta hiyo Mpya.
Alisema Zanzibar hivi sasa iko mbioni kujiandaa na uanzishaji wa
miradi ya Kiuchumi kupitia sekta ya Mafuta na Gesi ambayo Oman inaweza
kusaidia Taaluma kwa vile Nchi hiyo tayari imekuwa mzalishaji mkubwa wa
Nishati hizo kwa muda mrefu.
Naye Balozi Mdogo Mpya wa Oman aliyepo Zanzibar Dr. Ahmed Humoud Al –
Habsi alimuahidi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba Nchi yake
itaendelea kushirikiana na Zanzibar katika kuona uhusiano wa kidugu
uliopo baina nchi mbili unazidi kuimarika.
Alisema ahadi iliyotoa Oman kwa Zanzibar katika kugharamia
matengenezo makubwa ya Ujenzi wa Jengo la Jumba la Ajabu Forodhani
Mjini Zanzibar itatekelezwa kama ilivyopangwa.
Alimfahamisha Balozi Seif kwamba matayarisho ya utengenezaji wa
Jengo hilo hivi sasa yako tayari na ameahidi kufuatilia mitakaba
iliyofikiwa ili kuona kazi rasmi ya ujenzi huo inaanza bila ya kupoteza
wakati.
Dr. Ahmed Humoud Al – Habsi anaiongoza Ofisi ya Ubalozi Mdogo wa
Oman Zanzibar kufuatia aliyekuwa akishikilia nafasi hiyo Balozi Ali
Abdalla Al – Rashid aliyefariki Dunia ghafla mwezi Mei mwaka 2016
baada ya kusumbuliwa na tatizo la sindikizo la Damu { Blood Presure }.
Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali
Iddi alifanya ziara ya kulikagua jengo la Mashariki Hoteli liliopo
Pembezoni mwa Skuli ya Msingi Forodhani Mjini Zanzibar.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Uhifadhi wa Mji Mkongwe wa Zanzibar
Said Sarboko Makarani alimueleza Balozi Seif kwamba Serikali kupitia
Wizara inayosimamia Ujenzi ililikabidhi jengo hilo kwa Mamlaka hiyo
baada ya kukaa kwa zaidi ya miaka 25 bila ya kutumiwa.
Mkurugenzi Sarboko alisema matengenezo ya Miaka Miwili ya jengo hilo
yalianza mnamo mwaka 1985 ambapo baadaye mwaka 1987 ikalikodisha
kutumiwa kama Hoteli ya Kimataifa.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
chanzo: zanzibar24.
Comments