Wizi, ulevi wawaweka roho juu wazazi, Mwambe.


 Image result for ulevi

WIZI wa kupindukia, ulevi na ukiukwaji wa maadili unaofanywa na baadhi ya vijana wa shehia za Mwambe na Jombwe wilaya ya Mkoani Pemba, unaendelea kuwakosesha usingizi wazazi na walezi wa shehia hizo na kuanza kuomba misaada kutoka shehia nyengine.

Wazazi hao walisema, katika miaka ya hivi karibuni vijana wao ambao walikuwa mfano wa kufuata maadili, sasa hali imebadilika na kuanza kutishia maisha yao.

Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa nyakati tofauti, wazazi na walezi hao walisema vijana kwenye shehia hizo, wamekuwa wakiongoza kwa uvutaji wa bangi, wizi na ulevi.

Mmoja kati ya wananchi hao Haji Mcha, alisema suala la kuwakuta vijana wa Mwambe wakivuta bangi ni jambo la kawaida, ingawa hapo awali halikuwepo.

“Sasa hapa kwetu harufu na moshi wa bangi ni jambo la kwaida, maana vijana wameanzisha nyumba maalum za kuendesha vitendo vya kiharamia’’,alisema.

Nae Mwamize Makame Kombo, alisema uvutaji wa bangi umekuwa ukiambatana na wizi wa kuku, mbuzi na mazao jambo linalowakosesha usingizi wakulima na wafugaji.

Aidha Aisha Bakame Hamad alisema juzi kuku wake nane waliibiwa ndani ya siku tatu, sawa sawa na jirani yake alieibiwa idadi kama hiyo ndani ya mwezi mmoja.

“Mimi hamu ya kufuga kuku sinayo tena, maana vijana ambao ni watoto wetu, wamekuwa wakiwatega fyuka kuku, ili wapate wanunue sigara na ulevi’’,alieleza.

Katika hatua nyengine wananchi hao, walisema iwapo utamkamata mwizi na kumtolea taarifa mtaani, hugeuka na kufanya hujuma ya vipando.

“Ukimkuta anakubia ndizi, kuku au jambo lolote usalama wako ni kukaa kimnya, akijua kua umemnadia anakukatia mazao yako’’,alisema Kheir Makame.

Alieleza kuwa, hakuna hatua yoyote iliochukuliwa, hadi sasa na wazee hao, kutokana na wale wazazi wa wenye watoto wakorofi huwalinda watoto wao.

“Juzi kulikuwa na ugomvi wa ndugu, kwa mtoto wa mmoja kukamatwa na ndizi na kuku, na aliebiwa kumtaka kaka yake amkataze mwanae, basi waligombana akidai mwanae anazuliwa wizi tu’’,alisema.

Sheha wa shehia ya Jombwe Mwambe Hakim Khamis Omar, alikiri kuwepo kwa vitendo hivyo, ambavyo wastani kila mwezi hupokea kesi nne (4) za wizi.

“Wizi kwenye shehia yangu upo, na sasa pamoja na wizi wa Mbuzi, kuku lakini sasa vijana wamekosa woga maana wanadiriki hata kupindukia nyumba na kuiba watakachokikuta kama vile simu na fedha’’,alifafanua.

Kufuatia kukithiri kwa wizi huo wa mifugo sheha huyo, aliwakumbusha wananchi wake wasinunue wala wasiuze bidhaa yoyote pasi na risiti za serikali.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Kusini Pemba Shehan Mohamed Shehan, amewataka wazazi na walezi wa shehia hizo, kushirikiana na hata makao makuu ya Polisi, ili kusaka dawa ya kukomesha matendo hayo.

Alisema shehia zote 62 za Pemba zimeshaanzisha Polisi jamii, kwa lengo la kupunguza matendo hayo ya kihalifu, hivyo kama hali wanaihisi inaelekea kuwashinda, waripoti makao makuu kuomba msaada wa kiulinzi.

“Mwambe na Kengeja tumewawekea kituo cha Polisi, lakini wakihisi walinzi walioko huko wanasua sua, basi waripoti kwetu kulitafitia dawa jambo hilo kwa vijana wao”,alifafanua.   

Hivi karibuni Mkuu wa wilaya ya Mkoani Hemed Suleiman Abdalla, akizungumza na wananchi wa Kiwani, aliwataka kushirikiana ili kulinda vijiji vyao.

Katika miaka ya hivi karibuni shehia za Mwambe na Jombwe wilaya ya Mkoani Pemba, kumeibuka vitendo vya wizi na uvutaji wa bangi kwa vijana wanaosihi shehia hizo na kuwakosesha amani wazazi na walezi wao.

 chanzo:pembanewsz.

Comments