Ameonya kuwa kuwa askari yeyote aliyefukuzwa katika jeshi lingine
haruhusiwi kujiunga na taasisi yoyote iliyo chini ya Wizara ya Maliasili
na Utalii kwa kuwa wengi wao wamebainika kuwa si waminifu na wanaweza
kuitia doa wizara hiyo.
Milanzi ametoa onyo hilo jana wakati akifunga mafunzo ya wahitimu wa
mafunzo wa kutoka katika mfumo wa kiraia kwenda Jeshi Usu kwenye Kituo
cha Mafunzo kilichopo katika Makao Makuu ya Pori la Akiba la Rukwa –
Lwafi wilayani Mlele katika Mkoa wa Katavi.
Mafunzo hayo ya mwezi mmoja yaliyowashirikisha askari viongozi 133 wa
Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa) na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongo
(NCCA). Katika hafla hiyo, wahitimu walikula viapo vya utii na
kutunukiwa ngazi za kiuhifadhi ili wafanye kazi kwa kufuata mfumo wa
Jeshi Usu.
Katibu Mkuu alisisitiza kuwa uajiri katika taasisi zilizo chini ya
wizara hiyo utazingatia uzalendo, uaminifu ambapo anayeajiriwa awe na
uwezo wa kufundishika na kuwa na uhusiano mzuri na wananchi.
Alisema kwa miaka ya hivi karibuni nidhamu ya kazi katika taasisi
zilizopo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii imeporomoka kwa kasi
kubwa inayoashiriwa na visa ambavyo sio vya kiaskari na kiutumishi.
Aliwataka wahitimu wa mafunzo hayo ambao ni viongozi wa askari
wasaidie kurudisha nidhamu ya kazi kwa askari walio chini yao kwa
kuwaelekeza mambo mazuri ya kujenga.
Alitahadharisha kuwa kwa sasa hivi za taifa na mapori yote
yanakabiliwa na changamoto kubwa, ikiwemo uwindaji haramu wa wanyama
wakubwa wakiwemo tembo na faru kwa ajili ya pembe na vipusa na uingizaji
wa mifugo hifadhini.
Alisisitiza kuwa ni matarajio yake kuwa wahitimu hao baada ya kupata mafunzo hayo hifadhi za taifa nchini zitakuwa salama.
“Hili linategemea moyo wa uzalendo na ari ya kujituma kwenu kwa
kutumia mbinu mlizopata kuhakikisha kuwa mnatatua changamoto zilizo
katika maeneo yenu ya kazi,” alisisitiza.
chanzo:habarileo.
Comments