aziri Mkuu
Mstaafu, Jaji Joseph Warioba amelizungumzia sakata la vita ya dawa za kulevya
na kuvitaka vyombo vya habari na viongozi watoe elimu na kufanya utafiti wa
kina ili kupata suluhisho la tatizo hilo.
Akizungumza na
Mwananchi jana Jumapili, Jaji Warioba alisema ni wakati mwafaka kwa kila mmoja
kusoma sheria kuhusu makosa ya uuzaji na utumiaji wa dawa za kulevya na
kuvitaka vyombo vya habari viichambue kuangalia kama inafaa au ina mapungufu.
“Jamii isi-
‘dili’ na watu walioathirika tu, mnafikiri suala ni kumfunga anayetumia dawa za
kulevya au anayefundishwa kutumia dawa za kulevya?” alihoji.
Alisema kama ni
utafiti ufanyike kwa wanaosababisha na walioathirika badala ya kujikita na
matamko ya viongozi ambayo alisema hayasaidii kulimaliza tatizo hilo.
Jaji Warioba
ambaye pia alikuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, alisema ni vyema
kama wananchi wakaelekezwa wafanye nini ili kupambana na tatizo hilo badala ya
kujikita katika siasa na watu.
Alisema kwa kuwa
kuna sheria inayoeleza tatizo ni nini na kuna utaratibu wa namna ya kuitumia,
basi wananchi wangefundishwa ili wafahamu kitakachowasibu pindi
watakapojihusisha na dawa hizo haramu.
Alisema itafutwe
njia ya kushughulikia tatizo la dawa za kulevya badala ya kulumbana na kutoa
matamko kwani hayasaidii kumaliza tatizo.
Sakata la dawa
za kulevya liliibuliwa hivi karibuni na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul
Makonda baada ya kutaja orodha ya watu wanaodaiwa kutumia au kujihusisha na
biashara ya dawa hizo.
Orodha hiyo
iliyotolewa katika vipindi viwili tofauti, Februari 3 na Februari 13
ilijumuisha majina ya wasanii, viongozi wa kisiasa na wafanyabiashara wakubwa.
Miongoni mwa
waliotajwa katika orodha hiyo ni Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe,
mfanyabiashara maarufu na mwenyekiti wa klabu ya soka ya Yanga, Yusuf Manji na
Mchungaji wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima pamoja na msanii wa
filamu, Wema Sepetu.
Mtindo wa
Makonda kutaja majina ya watu uliibua mjadala mzito ambapo baadhi ya wabunge
walikosoa kitendo hicho wakidai kuwa ni cha udhalilishaji.
Aidha Jaji
Warioba hakupendezwa na jinsi vyombo vya habari nchini vilivyolishikia bango
suala la dawa za kulevya na kulihusisha na siasa na kusema kwamba wapo viongozi
wengi waliotajwa majina yao kwenye kashfa mbalimbali kipindi cha nyuma na
kuharibiwa heshima lakini vyombo vya habari viliona ni mambo ya kawaida.
“Hebu niwaulize,
hii ni mara ya kwanza kwa majina kutajwa? Tukianzia ‘list of shame,’ si
viongozi waliharibiwa heshima? Mbona hatukuona vyombo vya habari kuwatetea wale
walioharibiwa heshima? Kuna viongozi wengi waliharibiwa heshima lakini haikuwa
ishu, leo hii kumezidi nini mpaka kutajwa hao waliotuhumiwa kujihusisha na dawa
za kulevya imekuwa ishu?” alihoji.
Alisema wapo
viongozi (bila kuwataja) waliowahi kumuita Rais ni kuwa ni uchwara, wengine
walimuita dhaifu lakini halikuwa jambo la ajabu.
“Mnasema heshima
ya mtu imeharibiwa, je, kumuita rais ni uchwara si ni kumharibia heshima yake?”
alihoji.
Alisema
linapokuja suala kubwa la kupambana na dawa za kulevya, tatizo lenyewe
linakwepwa na watu wanaanza kuibua malumbano.
“Hivi mkimjadili
Makonda inawasaidia nini au kama kuna wanaomuunga mkono Makonda na wasiomuunga
mkono itawasaidia nini?” alihoji Jaji Warioba.
Pia Jaji huyo
alisema kuwa nchi ina matatizo mengi lakini watu wamejikita katika siasa tu.
Alisema hadi
bungeni walisema wamedhalilishwa lakini na wao huko nyuma walitoa matamko ya
kudhalilisha wenzao na hata kumhusisha rais na dawa za kulevya.
Ni vita ya
kimataifa.
Aliyekuwa
Kamishna wa Kitengo cha Dawa za Kulevya nchini, Alfred Nzowa alizungumzia vita
hiyo na kusema ni vyema taarifa za watu wanaotuhumiwa kujihusisha na dawa za
kulevya kwa namna yoyote zifanyiwe kazi kwanza kabla ya hatua yoyote.
“Hata Kamishna
wa sasa Sianga (Rogers) alisema hili, ni wazo zuri kupata taarifa na kuzichuja
na kuangalia kama zina ukweli,” alisema.
Hata hivyo Nzowa
alitoa siri ya kufanikiwa katika vita hiyo kuwa ni kuangalia mipaka mikubwa ya
kimataifa badala ya nchi au mtu mmoja kufanya peke yako bila kushirikiana na
wenzako.
“Kama ni
usafirishaji si ndani ya nchi hii moja, inapita nchi nyingi ni
‘Trans-organizational Syndicates.’ Wafanyabiashara hii ni wazuri katika
mawasiliano hivyo ni lazima anayefanya vita hii avunje mtandao,” alisema.
Alisema vita
vinaanzia huko inakolimwa na hivyo ni vyema kubadilishana uzoefu, mbinu na
majina ya wauzaji.
Pi alisema
katika kupambana na biashara hii ni lazima wanaopambana wawe na nguvu za ziada,
mikakati mipana na nidhamu kwani mapapa wa dawa hizo ni watu hatari.
chanzo:Mwananchi.
Comments