
Akizungumza katika mkutano huo unaofanyika Zanzibar Beach Hotel
Mbweni, Mkurugenzi Kinga na Elimu ya Afya Zanzibar Dkt. Fadhil Mohd
Suleiman amesema maradhi ya polio sio tatizao Tanzania kwa sasa, lakini
bado hatupo salama kutokana na nchi jirani kuendelea kusumbuliwa na
maradhi hayo.
Amesema Tanzania mara ya mwisho kuwa na mgonjwa wa polio ni mwaka
1997 lakini nchi ya Somalia, Jamhuri ya Watu wa Kongo na Nigeria bado
wanakabiliwa na maradhi hayo na watu wake wanakuja kwa shughuli mbali
mbali za maisha hivyo matayarisho ya kujiandaa ni jambo muhimu.
Amewashauri wazazi kuendelea na utaratibu wa kuwapeleka watoto wao
katika vituo vya afya mara baada ya kuzaliwa kupatiwa chanjo zote ili
kuhakikisha maradhi hayo na mengine yanayowasumbua hayarejei tena.
Meneja wa Kitengo cha chanjo Zanzibar Dkt. Yussuf Haji Makame amesema
hali ya chanjo iko vizuri baada ya asilimia 95 ya watoto wanaostahiki
kupatiwa chanjo kupatiwa chanjo hizo.
Amesema kitengo hivi sasa kinaendelea kufuatialia kwa karibu watoto
wenye umri kuanzia miaka 15 wanapopata ulemavu wa ghafla ili kujua
chanzo chake na amewataka wazee wanapobaini kijana wao kupata tatizo
hilo kumpeleka hospitali mapema.
Mwakilishi wa WHO Zanzibar Dkt. Andemichael Ghirmay ameipongeza
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa juhudi kubwa za kupambana na polio na
kufanikiwa kupewa cheti maalumu mwaka 2015.
Amesema Shirika hilo litaendelea kuunga mkono juhudi zinazoendelea
kuchukuliwa na serikali na ametaka juhudi za pamoja za wadau na jumuiya
za kimataifa kuhakikisha polio na maradhi mengine yanayozuilika kwa
chanjo sio tatizo tena Zanzibar.
Akifungua mkutano huo Katibu Mkuu Wizara ya Afya Bi. Asha Abdalla
amewataka wadau wa chanjo kutoridhika na hatua iliyofikiwa ya kutokomeza
Polio bali waendelee kuweka mikakati bora zaidi itakayo hakikisha
maradhi hayo hayarejei.


Comments