UN: Mamilioni ya watu wanakabiliwa na baa la njaa Nigeria, Ziwa Chad.

Umoja wa Mataifa umeripoti kuwa, zaidi ya watu milioni saba wanakabiliwa na hatari ya baa la njaa katika eneo lililokumbwa na machafuko la kaskazini mwa Nigeria na kandokando ya Ziwa Chad.

Mratibu wa Misaada ya Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa, Toby Lanzer amesema kuwa, watu milioni saba katika maeneo hayo wanakabiliwa na hatari kubwa ya njaa na kwamba wanadhamini mlo mmoja kwa siku kwa tabu kubwa. Amesisitiza kuwa njaa ndiyo inayotiwa wasiwasi mkubwa kuhusu hali ya watu eneo hilo.

Lanzer amesema kuna wasiwasi kwamba kundi la kigaidi la Boko Haram litawazuia raia kulima mazao ya chakula baada ya kukosa kulima kwa misimu mitatu na kwamba suala hilo litazidisha hali mbaya katika maeneo ya kaskazini mwa Nigeria na kandokando ya Ziwa Chad.
Afisa huyo wa Umoja wa Mataifa pia amesema hali ya raia waliokimbia makazi yao huko kaskazini mwa Nigeria inatia wasiwasi na kwamba yumkini wakaathiriwa na msimu wa mvua kali.
Toby Lanzer ametoa wito wa kuzidishwa misaada ya chakula, pembejeo na kadhalika kwa ajili ya wakimbizi na wakazi wa maeneo hayo.
Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa, watu wawili kati ya kila watatu miongoni mwa wakazi milioni 10.7 wa kaskazini mwa Nigeria wanahitajia misaada ya kibinadamu.
chanzo:parstoday.

Comments