Rais Dkt Magufuli aeleza kusikitishwa kwake na namna mahakama inavyoshughulikia kesi za ukwepaji kodi.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli
ameelezea kusikitishwa kwake na namna Mahakama inavyoshughulikia kesi
zinazohusiana na ukwepaji wa kodi na ametoa wito kwa mahakama na wadau
wake kujipanga kukabiliana na dosari hiyo inayorudisha nyuma juhudi za
maendeleo ya nchi.
Mhe.
Rais Magufuli ametoa kauli hiyo leo tarehe 02 Februari, 2017 katika
sherehe za uzinduzi wa mwaka wa Mahakama (Siku ya Sheria) zilizofanyika
katika uwanja wa Mahakama uliopo Mtaa wa Chimala, Kivukoni Jijini Dar es
Salaam na kubainisha kuwa katika kipindi cha kuanzia mwaka 2005 hadi
mwaka 2016 Serikali haijalipwa kiasi cha Shilingi Trilioni 7.5 licha ya
kushinda kesi za ukwepaji kodi zilizokuwa zinawakabili washitakiwa
mbalimbali.
Dkt.
Magufuli ameipongeza Mahakama na wadau wake kwa kazi kubwa inayofanywa
kuleta mabadiliko na uboreshaji wa huduma na miundombinu na ametaka
kauli mbiu ya mwaka huu isemayo “Umuhimu wa utoaji wa haki kwa wakati
kuwezesha ukuaji wa uchumi” itekelezwe vizuri kwa kutanguliza maslai ya
Taifa ikiwemo kuhakikisha wanaopatikana na hatia ya kukwepa kodi
wanalipa.
“Haiwezekani mwekezaji anachimba madini yetu, kodi halipi, anashitakiwa mahakamani anashindwa, halafu pesa haitolewi.
“Sasa
tujiulize, kama utoaji haki unaakisi ujenzi wa uchumi wa nchi ni kwa
kiasi gani kesi zenye thamani ya Shilingi Trilioni 7.5 zimeathiri
uchumi?” amehoji Mhe. Rais Magufuli.
Aidha,
Mhe. Rais Magufuli ametaka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP),
Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Polisi, Taasisi ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na Mahakama wajipange kwa pamoja ili
kushughulikia ipasavyo mashauri mbalimbali na kuondokana na migongano
ambayo imekuwa ikidhohofisha ufanisi wa shughuli za kimahakama.
Pia Dkt. Magufuli ameahidi kushughulikia tatizo la ufinyu wa bajeti na maslai ya wafanyakazi wa Mahakama wakiwemo Majaji.
Pamoja
na kumpongeza na kumshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa ushirikiano mkubwa
anaoutoa kwa Mahakama, Kaimu Jaji Mkuu wa Mahakama Tanzania Mhe. Prof.
Ibrahim Juma amesema katika kutekeleza Mpango Mkakati wa Mahakama, mwaka
2016 jumla ya mashauri 279,331 yamesikilizwa sawa na asilimia 101 ya
matarajio ya kusikiliza mashauri 276,147, Mahakama imefanikiwa kumaliza
kesi 248 kati ya kesi 249 za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 zilizohusisha
Ubunge na Udiwani na pia Mahakama Kuu imefanikiwa kuanzisha Divisheni ya
makosa ya rushwa na uhujumu uchumi (Mahakama ya Mafisadi)
Sherehe
hizo zimehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Spika wa Bunge la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Ndugai, Jaji Mkuu wa Zanzibar
Mhe. Omar Othman Makungu, Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Harrison
Mwakyembe, Katibu Mkuu Kiongozi Mhe. John Kijazi, Majaji wa Mahakama ya
Rufani, Jaji Kiongozi Mhe. Ferdinand Leons Wambali, Majaji wa Mahakama
Kuu, Mawakili, Viongozi wa Dini na Siasa na wawakilishi wa Taasisi
mbalimbali.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
02 Februari, 2017
chanzo:mpekuziblog.
Comments