
Dk. Shein aliyasema hayo leo Ikulu mjini Zanzibar wakati alipofanya
mazungumzo na Balozi wa Urusi katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Yuri Fedorovich Popov ambapo katika mazungumzo hayo balozi huyo
alimuahidi Dk. Shein kuwa Urusi itazidisha uhusiano na ushirikiano kati
yake na Zanzibar.
Katika maelezo yake Dk. Shein alisema kuwa ipo haja ya kuimarisha
zaidi uhusiano na ushirikiano huo uliopo kati ya nchi hizo kwa kutambua
kuwa thamani yake ni kubwa katika maendeleo kwa pande zote mbili.
Dk. Shein alisema kuwa Urusi ni nchi moja wapo inayotoa watalii wengi
duniani ambao sio wengi wanaozitembelea nchi za Bara la Afrika ikiwemo
Tanzania, hivyo alisisitiza haja ya mashirikiano ya pamoja kati ya pande
mbili hizo katika kuifanyia kazi sekta hiyo ambayo nimuhimukatika
kukuza uchumi na maendeleo hapa nchini.
Dk. Shein aliongeza kuwa kurejea huduma za usafiri wa ndege kati ya
Tanzania na Urusi kama ilivyokuwa hapo siku za nyuma kupitia Shirika
lake la ndege la “Aeroflot”, kutasaidia kwa kiasi kikubwa
kuikamarisha sekta ya utalii hapa nchini kwani itasaidia kuleta watalii
kutoka nchi hiyo moja kwa moja.
Sambamba na hayo, Dk. Shein alimueleza Balozi huyo haja ya kuendeleza
na kuongeza nafasi za masomo kwa vijana wa Zanzibar wanaokwenda nchi
hiyo kwa ajili ya kusoma katika kada mbali mbali za elimu ya juu.
Akizungumzia kuhusu sekta ya biashara, Dk. Shein alisema kuwa
Tanzania ikiwemo Zanzibar ina historia kubwa katika sekta ya biashara
kati yake na Urusi hivyo ipo haja kwa hatua hiyo kurejeshwa kama
ilivyokuwa siku za nyuma.
Aidha, Dk. Shein aliipongeza Serikali ya Urusi kwa kuendeleza
uhusiano na ushirikiano wa karibu kati yake na Zanzibar na kueleza kuwa
nchi hiyo ni miongoni mwa nchi za mwanzo kufungua Ubalozi wake hapa
Zanzibar mara tu baada ya Mapinduzi ya Januari 12, mwaka 1964.
Hivyo, Dk. Shein aliitilia mkazo rai ya Balozi Yuri Popov ya
kuimarisha uhusiano kama ilivyokuwa katika miaka ya 1970 na 1980 ambapo
Urusi iliimarisha zaidi uhusiano huo na Tanzania ikiwemo Zanzibar kwani
pia, nchi hiyo ni miongoni mwa nchi za mwanzo kuyatambua Mapinduzi ya
Zanzibar ya Januari 12, 1964.
Nae Balozi wa Urusi katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Yuri
Fedorovich Popov alimuhakikishia Dk. Shein kuwa Urusi itaendelea
kushirikiana na kuiunga mkono Zanzibar kwa kutambua uhusiano na
ushirikiano mwema wa kihistoria uliopo.
Katika maelezo yake, Balozi Yuri alieleza kuwa Urusi inatambua
umuhimu wa kuimarisha uhusiano na ushirikiano huo ambao utakuza
maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa pande zote mbili.
Kwa upande wa sekta ya utalii, Balozi Popov alieleza kuwa juhudi za
makusudi zitachukuliwa katika kuhakikisha usafiri wa ndege kati ya Urusi
na Tanzania utarejeshwa ili kukuza sekta hiyo ya utalii pamoja na sekta
ya biashara na shughuli za uwekezaji.
Alieleza kuwa kwa upande wa sekta nyengine za maendeleo nchi yake
itaongeza nguvu zaidi katika kuhakikisha mafanikio zaidi yanapatikana
katika sekta hizo ili kuimarisha uchumi na maendeleo kwa nchi mbili
hizo.
Pamoja na hayo, Balozi Popov alitumia fursa hiyo kumpongeza Rais Dk.
Shein kwa kuendelea kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi kwa kipindi cha Pili pamoja na kuwapongeza wananchi wa
Zanzibar huku akiahidi kuwa wananchi wa Urusi wataendeleza ushirikiano
na ndugu zao wa Zanzibar.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
CHANZO: zanzibar24.
Comments