Mganga Mkuu wa Hospitali ya Benjamin Mkapa wilayani hapa, Dk Said Mawji amekiri kupokea miili ya watu wanne na majeruhi wawili.
Dk Mwaji aliwataja waliokufa kuwa ni Maritha Mabula (60), Shukuru
Donald (15) mwanafunzi wa kidato cha pili katika Shule ya Sekondari
Mwana Kianga na Bernadeta Mabula(7) mwanafunzi wa darasa la kwanza Shule
ya Msingi Ilolo na mwingine ni Jeska Lubeleje (19) mkazi wa Kijiji cha
Chinyika katika Kata ya Vighawe.
Aliwataja majeruhi wawili waliojeruhiwa kwenye ajali hiyo ni Beka
Mlami na Joseph Sumisumi. Aidha, alisema kwamba majeruhi wametibiwa na
kuondoka.
Alieleza kuwa katika ajali hiyo, mmoja wa watoto walionusurika na
kifo Beca Mrami (10), alisema maji yaliingia ndani ya nyumba na
akalazimika kukimbilia darini na ndugu yake, lakini walipoona yamezidi
walikimbia wakimwacha bibi yao na dada zake.
“Mimi nilipoona maji yanazidi nikawaambia tukimbie, lakini bibi na
akina dada walibaki ndani; mimi na Mandili (Joseph Sumisumi ) tulipanda
juu ya paa baada ya nyumba kuanguka nilikimbia na kuwaacha ndani,”
alieleza mtoto huyo.
Mzee wa kaya hiyo, Mabula Sumisumi, alisema hakuwapo katika mji huo
siku hiyo alienda kulinda mifugo kambini ndipo alipoambiwa familia yake
imesombwa na maji.
Hata hivyo, Sumisumi alisema kila kitu kilichokuwamo ndani kimesombwa
na maji ikiwamo akiba ya chakula na fedha kiasi alizokuwa amehifadhi
ndani ya nyumba ambazo hakuzitaja kiasi chake.
Shuhuda wa tukio hilo, Simon Kazimoto alisema nyumba hiyo imesombwa
kutokana na kuwa ilijengwa kwenye mkondo wa maji na kutokana na
uharibifu wa mazingira unaoendelea umesababisha maji kutawanyika na
kuingia katika makazi ya watu na kusababisha vifo.
Katibu wa Kamati ya Ulinzi na Usalama, Said Kilungo alisema kwa hatua
za awali zilizochukuliwa na serikali ni kuhifadhi maiti kwa kugharamia
jeneza na sanda kwa kila maiti baada ya hapo hatua zaidi zitafuata.
Kilungo aliwataka wananchi wa kitongoji hicho kuhama katika maeneo
hatarishi kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha kwa sasa.
Pamoja na mvua hiyo, kusababisha vifo vya watu wanne, lakini tayari
baadhi ya miundombinu ya Wilaya ya Mpwapwa iko hatarini kusombwa na
maji, ikiwamo daraja la Tanesco na daraja la kwenda Ofisi ya Mkuu wa
Wilaya.
chanzo:habarileo.
Comments