
Gari hilo lenye thamani ya Sh milioni 200, ni miongoni mwa magari 50
yaliyotolewa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto kupitia Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa mikoa ya Kanda ya Ziwa.
Gari hilo la wagonjwa limekabidhiwa jana katika hafla iliyofanyika
katika kituo hicho ambalo litakuwa ni msaada mkubwa kwa wakazi wa eneo
hilo kutokana na hapo awali walikuwa wanapata usumbufu pindi wanapoumwa
kutokana na upatikanaji wa gari kuwa mgumu.
Akizungumza na wananchi wa tarafa hiyo baada ya kukabidhi msaada wa
gari hilo la wagonjwa, Ndaki alisema magari kama hayo yametolewa katika
maeneo mbalimbali ya nchi hasa mikoa ya Kanda ya Ziwa na gari moja pekee
ndilo limetolewa kwa wananchi wa jimbo hilo.
Aliipongeza Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli
ambayo iliahidi kutatua changamoto ya kero ya vifo vya wajawazito
ambavyo vilikuwa vikitokea kutokana na eneo hilo kukosa gari la
wagonjwa.
“Kutokana na huduma hafifu ya rufaa kwa wajawazito kwa kukosa magari
ya wagonjwa, ukosefu wa damu salama na ushiriki mdogo wa jamii katika
mambo yanayohusu afya ya mama, ikiwemo kutotambua dalili hatari wakati
wa ujauzito za kuokoa maisha ambayo yanachangia wingi wa vifo
vitokanavyo na uzazi hivyo serikali imeona umuhimu wa kutupatia gari
hili,” alisema mbunge huyo.
Alisema shida waliyokuwa wakiipata kwa muda mrefu wananchi wa tarafa
hiyo hasa ya usafiri pindi wanapokuwa wagonjwa na wengine kusafirishwa
kwa kutumia magari ya kukodi kwa Sh 120,000 huku wengine wakilazimika
kutumia matela yanayokokotwa na ng’ombe, sasa itakuwa historia.
Aidha, aliongeza kuwa nia yake kubwa mbali na kupata msaada huo wa
gari la wagonjwa pia atahakikisha anaboresha sekta ya afya katika jimbo
katika zahanati na vituo vyote vya afya ili kuwapa fursa wananchi wapate
huduma ambayo inastahili pamoja na matibabu.
Pia alisema anapambana vilivyo kuhakikisha kunakuwepo na vifaa vya
tiba katika maeneo husika pamoja na kuongeza idadi ya wauguzi, kwani
anatambua bado kuna changamoto nyingi katika sekta ya afya hivyo
atajitahidi kadiri ya uwezo wake ili kuongeza kasi ya kuboresha huduma
hiyo ya afya.
Mkazi wa Kijiji cha Malampaka, Jamila Hamis aliishukuru serikali
kutokana na kuwepo kwa kilio cha siku nyingi cha wananchi kutozwa
gharama kubwa ya usafiri.
“Leo serikali imesikia kilio chetu cha muda mrefu kwani tulikuwa
tunatozwa kiasi kikubwa cha fedha kati ya shilingi laki moja hadi
shilingi laki moja na ishirini kwa kutumia magari ya watu binafsi pindi
unapokuwa na mgonjwa unapotakiwa kumleta katika kituo chetu cha afya au
hata akipata rufaa ya kupelekwa katika Hospitali ya Wilaya ya Maswa
ambayo iko umbali wa kilometa thelathini na nane. Sasa kuanzia mwezi huu
hiyo kilio hicho hakitakuwepo tena,” alieleza.
Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Dk Vedastus Luguga alisema
kipindi cha nyuma wagonjwa walikuwa wanapata shida kubwa ya usafiri na
wakati mwingine walishindwa kwenda kupatiwa matibabu kwa muda wa muafaka
na kusisitiza kuwa hakuna mwananchi yeyote atakayetozwa gharama katika
kutumia gari hilo.
chanzo:Habarileo.
Comments