Maalim Seif apania kuifuta CCM Pemba, Vuai amjibu.

Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim
Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad ameahidi kuwa chama chake kitahakikisha kinaibomoa ngome yote ya CCM Pemba kwa kuwashawishi wanachama wake kukihama.



Hata hivyo, alipotakiwa kutoa maoni yake juu ya kauli hiyo ya Maalim Seif jana, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai alisema makamu huyo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar katika Serikali iliyopita hana uwezo wa kuidhoofisha CCM Pemba kwa kuwa chama chake kina msingi imara na wananchi wake wanakikubali.


“Uwezo aliokuwa nao Maalim Seif ni kufukuza viongozi ndani ya chama chake kazi anayoifanya kila siku,” alisema Vuai.


Maalim Seif alisema hayo juzi alipokuwa akitoa kadi kwa wanachama wapya 2,240 waliojiunga na CUF kutoka maeneo ya Kiuyu Minungwini, Kilindini Mapofu na Tumbe Wilaya ya Micheweni, Kaskazini Pemba akiwa katika ziara yake ya siku 1.



Mara baada ya kukabidhi kadi hizo, aliwaambia wanachama hao wapya kwamba wapo huru kufanya jambo lolote ambalo lipo kwa mujibu wa sheria na katiba ikiwamo kupiga kura na kuwania nafasi waitakayo.



Alisema hakuna mwanachama mwenye haki ya kikatiba ndani ya chama hicho atakayenyimwa haki hivyo kuwataka wasirudi nyuma.



Alisema kazi kubwa ya chama hicho hivi sasa ni mapambano dhidi ya dhuluma aliyodai ilifanywa na chama tawala dhidi ya CUF katika Uchaguzi Mkuu wa 2015.


Akizungumzia madai hayo, Vuai alisema hakuna dhuluma yoyote iliyofanywa na CCM dhidi ya CUF katika uchaguzi uliopita.


Wakizungumza mara baada ya kuhamia CUF, wanachama hao walisema lengo la kujiunga na chama hicho kikubwa cha upinzani visiwani imetokana na kuchoshwa na ahadi zisizotekelezeka.



Walisema ustahamilivu umewashinda hivyo wameamua kujiondoa CCM  bila ya kushurutishwa ili kuungana na walio wengi katika kudai haki yao nchini.


Sharifa Kamis Ali ambaye alikuwa Sheha wa Shehia ya Kiuyu kupitia CCM alisema pamoja na kufanya kazi hiyo kwa muda mrefu, hakuna alichokipata.



Alisema ndani ya chama hicho alikuwa anafanya kazi bila ya kujiamini huku faida kubwa ikiwa ni kwa viongozi wakuu na kuwaacha wa chini wakihangaika na ulimwengu.


chanzo:Mwananchi.

Comments