Dk. Shein aliyasema hayo mara baada ya kukabidhiwa Ripoti ya
Uchaguzi Mkuu wa tarehe 25 Oktoba 2015 pamoja na Uchaguzi wa Marudio wa
terehe 20 Machi mwaka jana,
Ripoti ambayo ni kwa ajili ya Uchaguzi wa
Rais wa Zanzibar, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na Madiwani.
Hafla hiyo, ilifanyika Ikulu mjini Zanzibar na kuhudhuriwa na
viongozi mbali mbali akiwemo Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi
Seif Ali Idd, Jaji Mkuu wa Zanzibar Omar Makungu, Spika wa Baraza la
Wawakilishi Zubeir Ali Maulid, Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar Said Hassan,
Mawaziri, Washauri wa Rais, Wajumbe wa Tume hiyo na viongozi wengine wa
Serikali.
Katika maelezo yake Dk. Shein alisema kuwa Ripoti hiyo ni muhimu sana
katika utekelezaji wa kazi za Serikali na kuipongeza Tume ya Uchaguzi
pamoja na viongozi wake wote kwa kazi nzuri ya kutayarisha Ripoti hiyo
kwa umakini mkubwa na busara pamoja na hekima kubwa.
Dk. Shein alitumia fursa hiyo kutoa pongezi kwa wananchi wa Zanzibar
kwa kushiriki uchaguzi wa kwanza wa Oktoba 25 mwaka 2015 pamoja na ule
wa marudio wa Machi 20 mwaka jana na kutumia haki yao ya kuwachagua
viongozi wanaowataka.
Aidha, Dk. Shein alisema kuwa Tume ya Uchaguzi inaongozwa na Katiba
ya Zanzibar ya mwaka 1984 pamoja na Sheria ya Uchaguzi Namba 11 ya mwaka
1984, hivyo aliwapongeza kwa kuzitumia nyenzo hizo kwa kutekeleza
majukumu yao kutokana na changamoto zilizojitokeza katika uchaguzi mkuu
wa Oktoba 25 mwaka 2015.
Dk. Shein alisema kuwa, kama inavyofahamika kuwa Tume hiyo
haiingiliwi na taasisi wala mtu yoyote hivyo Tume ndio inayojua ukweli
na hatimae ndio imetayarisha ripoti hiyo ambayo ina umuhimu mkubwa kwa
Serikali pamoja na wananchi wote.
Alisema kuwa kutokana na tukio hilo kuwa muhimu ndio maana amewaalika
Mawaziri wote wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuja kushuhudia
tukio hilo muhimu na kusisitiza kuwa mapendekezo yote anayakubali.
Sambamba na hayo, Dk. Shein alipongeza mashirikiano mazuri yaliopo
kati ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar na Tume ya Uchaguzi ya Taifa na
kutumia fursa hiyo kuwapongeza wale wote waliosaidia uchaguzi huo.
Dk. Shein alimueleza Mwenyekiti huyo wa Tume ya Uchaguzi kuwa,
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya uongozi wake italisimamia kwa
karibu suala la changamoto ya ofisi yao kwa kujengwa ofisi nyengine
mpya au kufanyiwa ukarabati iliyopo hivi sasa huku akiahidi kufanya
ziara siku ya Jumaatatu ili kujionea mwenyewe hali halisi ya ofisi hiyo.
Mapema Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar Jesha Salim Jecha
alieleza kuwa Ripoti hiyo inaeleza utaratibu wote wa Uchgauzi tangu
uandikishaji wa wapiga kura katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura,
mapitio ya uchaguzi wa idadi, majina na mipaka ya majimbo ya uchaguzi,
uteuzi wa wagombea.
Pia, Mwenyekiti Jecha alieleza kuwa Ripoti hiyo inaeleza kuhusu
kampeni, kupiga kura, kuhesabu kura hadi kutangazwa kwa matokeo na
uteuzi wa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Viti maalum.
Aidha, Mwenyekiti Jecha alisema kuwa Ripoti hiyo imeeleza kufutwa
kwa uchaguzi na matokeo yake pamoja na usimamizi wa uendeshaji wa
uchaguzi wa marudio mwaka 2016.
Aliongeza kuwa Ripoti ya Uchaguzi ni nyenzo muhimu sana itakayotumika
kutoa maelezo ya mchakato wa shughuli zote zilizofanywa katika kipindi
chote cha uchaguzi na kusisitiza kuwa uandishi wa Ripoti hiyo hauna
tofauti na ripoti nyengine zinazohusiana na Uchaguzi wa Rais, Wajumbe wa
Baraza la Wawakilishi na Madiwani kwa chaguzi zilizopita.
Ripoti hiyo yenye lugha ya kiswahili ina Sura 15, kurasa 302,
Majedwali 13 na Viambatisho 28 ambao kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo
Ripoti hiyo itasambazwa sehemu mbali mbali zikiwemo Ofisi na Taasisi za
Serikali na Mahkama.
Sehemu nyengine ni Baraza la Wawakilishi, Vyama vya Siasa, Maktaba ya
Taifa, Maktaba za Vyuo vya Elimu ya Juu, Idara ya Nyaraka, Taasisi
zisizo za Serikali pamoja na Wadau mbali mbali ambapo pia, itawekwa
kwenye tovuti ya Tume ya Uchaguzi.
Sambamba na hayo, Mwenyekiti huyo alitumia fursa hiyo kueleza
changamoto mbalimbali zinazoikabili Tume hiyo na kueleza kuwa Serikali
haina budi kusaidia ili kuzipatia ufumbuzi ikiwemo nafasi finyu katika
jengo la Ofisi za Tume hiyo.
Mwenyekiti Jecha alieleza kuwa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar inatoa
shukurani kwa wadau wote walioshiriki kwa namna moja au nyengine na
ambao kwa nafasi zao walisaidia kufanikisha uchaguzi huo.
Akiwataja miongoni mwao ni Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar,
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Tume ya Taifa ya Uchaguzi
(NEC), Shirika la Umoja wa Mataifa la Mipango ya Maendeleo (UNDP) na
Washirika wengine wa Maendeleo.
Wadau wengine aliowatajwa ni vyama vya siasa, asasi za kiraia, vyombo
vya habari vya ndani na nje ya nchi, waaangalizi wa uchaguzi wa ndani
na nje na wanancho wote wa Zanzibar.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
chanzo:zanzibar24.
Comments