
Dk. Shein aliyasema hayo leo mara baada ya kufanya
ziara fupi ya kulitembelea jengo la Ofisi za Tume ya Uchaguzi ya
Zanzibar huko Maisara mjini Zanzibar, ikiwa ni ahadi yake aliyoitoa hivi
karibuni wakati alipokabidhiwa
ripoti ya uchaguzi wa tarehe 25 Oktoba
pamoja na uchaguzi wa Marudio wa tarehe 20 Machi 2016 na Mwenyekiti wa
Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar Jecha Salim Jecha kuwa leo atazitembelea
Ofisi hizo.
Katika maelezo yake Dk. Shein alisema kuwa Tume zote za uchaguzi
duniani zipo katika mazingira na sehemu nzuri kwa kutambua kuwa chombo
kinachosimamia uchaguzi ni lazima kiwe katika mazingira mazuri
yanayoendana na hadhi yake hivyo, lazima Serikali ifanye juhudi za
kuhakikisha Ofisi za Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar inakuwa katika
mazingira mazuri.
Dk. Shein alisema kuwa ni vyema wakati uchaguzi wa mwaka 2020
ukiandaliwa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) iwe na Ofisi nzuri na
zenye nafasi kwa ajili ya kufanya kazi zao kwa ufanisi zaidi pamoja na
vifaaa na vitendea kazi imara yakiwemo magari na kuahidi kuwa Serikali
anayoiongoza itafanya juhudi katika kuhakikisha changamoto hiyo inapata
ufumbuzi.
Alisema kuwa kwa upande wa Tume ya Uchaguzi ya Taifa (NEC) tayari
inampango wa kujenga jengo lake huko Dodoma ambalo litakuwa na mazingiza
mazuri hivyo, kwa upande wa Zanzibar Ofisi hizo za Tume nazo ni vyema
zikawa zinaenda na wakati uliopo kwa kuwa na majengo yanayoendana na
hadhi ya Tume.
Kutokana na hilo, Dk. Shein aliahidi suala hilo kupatiwa ufumbuzi na
jawabu muwafaka litapatikana haraka iwezekanavyo na kusema kuwa wakati
wowote jibu muwafaka litapatikana kama Serikali itajenga jengo jipya ama
kufanyiwa ukarabati au upanuzi kwa majengo yaliopo sehemu hiyo likiwemo
jengo jengine pembezoni mwa Ofisi za Tume hizo ambalo halitumiki kwa
sasa.
“Nitafanya maamuzi leo na mchana huu tutakuwa na kikao na tutaamua na
kukuarifuni maamuazi tuliyoamua juu ya ujezi wa Ofisi ya Tume ya
Uchaguzi ya Zanzibar”,alisisistiza Dk. Shein.
Aidha, Dk. Shein alielendelea kuwasisitiza viongozi na wafanyakazi wa
Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar waendelee kufanya kazi zao na kujituma
huku akiwaahidi kuwa Serikali yao ya Mapinduzi ya Zanzibar ipo na
itaendelea kuwaunga mkono na wala wasiwe na wasi wasi.
Mapema Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, Jecha Salim Jecha
alitoa pongezi zake kwa niaba ya Tume hiyo kwa Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein kwa kufanya
ziara yake hiyo ya kuzitembelea Ofisi za Tume hiyo kutokana na ombi lake
alilolitoa kwa Rais hivi karibuni.
Mwenyekiti huyo wa Tume ya Uchaguzi alitumia fursa hiyo kueleza
changamoto wanazozipata kutokana na ufinyu wa nafasi katika ofisi zao
sambamba na mahitaji yao ya vifaa na vitendea kazi vyengine yakiwemo
magari.
Katika ziara hiyo Dk. Shein alitembelea sehemu mbali mbali za ofisi
hiyo na kupata maelezo kutokana na changamoto ya ufinyu wa nafasi za
ofisi za Tume hiyo, pia, alioneshwa kiwanja kiliopo pembeni ya jengo la
Tume hiyo pamoja na kukagua, jengo ambalo halitumiki kwa hivi sasa
ambalo liko pembezoni mwa ofisi za Tume hiyo.
Viongozi mbali mbali wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, waliungana
na Rais Dk. Shein katika ziara hiyo fupi ambayo pia, ni muhimu akiwemo
Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd, Mawaziri,
Makamishna na viongozi wengine wa Serikali.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar.
chanzo: zanzibar24
Comments