
Dk. Shein ambaye pia, ni Makamo Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, aliyasema
hayo huko katika ukumbi wa CCM, Mkoa wa Mjini uliopo Amani mjini
Zanzibar mara baada ya kukabidhi vifaa vya michezo kwa vijana kwa ajili
ya maandalizi ya Ligi ya Mpira wa Miguu kwa Timu 18 za Unguja ikiwa ni
kusherehekea miaka 40 ya kuzaliwa kwa CCM.
Katika hotuba yake Dk. Shein aliwataka vijana washindane katika
mchezo huo na wala wasigombane kwani lengo la michezo pamoja na
kuanzishwa kwa mashindano hayo ni kujenga umoja baina yao.
Dk. Shein aliwataka vijana hao wacheze vizuri ligi hiyo ili kuendelea
kukipa heshima na mapenzi chama chao cha CCM na kueleza kuwa Ilani ya
chama hicho ina vifungu vinavyoeleza kutekelezwa kwa sekta hiyo ya
michezo.
Aliongeza kuwa mashindano hayo yana lengo la kuimarisha chama, kutoa
vipaji kwa vijana na kuwataka viongozi wa Majimbo kuwaunga mkono na
kuwasaidia vijana wao watakaoshiriki katika ligi hiyo kwani na wao
wanawajibu wa kufanya hivyo.
Pia, Dk. Shein alikubali rai iliotolewa na Mwakilishi wa Jimbo la
Uzini ambaye pia, ndio mdhamini wa mashindano hayo Mohammed Raza ya
kuanzisha mashindano kama hayo kisiwani Pemba pamoja na mashindano ya
vijana katika skuli za Mikoa yote ya Zanzibar na kuahidi kuyadhamini kwa
kushirikiana na wahisani wengine wa michezo hapa nchini.
Dk. Shein ambaye aliongeza kuwa uzinduzi wa mashindano hayo
utafanyika tarehe 24 mwezi ujao kati ya Timu ya Mfenesini na Mpendae
mchezo utakaopigwa katika uwanja wa Amaan mjini Zanzibar.
Nae Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar ambaye pia, ni Mjumbe wa
Kamati Kuu ya CCM Balozi Seif Idd, alitumia fursa hiyo kueleza umuhimu
wa mashindano hayo kwa vijana na kusisitiza kuwa ligi hiyo itazidi
kukuza mashirikiano na umoja kwa vijana wa chama hicho.
Mapema Mdhamini wa mashindano hayo, Mohammed Raza alisema kuwa
mchakato wa kuanzishwa kwa mashindano ya ligi hiyo ni miongoni mwa
utekelezaji wa Ilani ya CCM sambamba na kutekeleza malengo ya
kuwatumikia wananchi na utekelezaji wa ahadi kwa wananchi.
Raza alisema kuwa kazi kubwa iliyopo hivi sasa ni kuwatumikia
wananchi bila ya ubaguzi na kusisitiza umuhimu wa mashirikiano ya pamoja
kwa wanaCCM ili kufikia malengo waliyojiwekea huku akieleza azma yake
ya mashindano hayo kuyapeleka kisiwani Pemba.
Katika taarifa ya Ligi hiyo iliyosomwa na Omar Suleimn, Mjumbe wa wa
Kamati ya Michuano hiyo, ilieleza kuwa Umoja wa Vijana wa CCM kwa
kushirikiana na CCM Mkoa wa Mjini, wameamua kuanzisha ligi ya Majimbo ya
Mpira wa miguu ambayo itashirikisha timu 18, Timu 9 kutoka Majimbo ya
Mkoa wa Mjini kichama, Timu ya Tawi la Afisi Kuu ya CCM, Timu ya CCM
Family na Timu zilizo salia zitatoka Mkoa wa Magharibi, Kusini na
Kaskazini Unguja.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa mara baada ya kupata wazo la kuanzisha
ligi hiyo, iliundwa Kamati ya maandalizi ya mashindano hayo yenye
Wajumbe 12 chini ya uongozi wa CCM Mkoa wa Mjini ambapo mshauri wa
Kamati hiyo Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Ayoub Mohammed Mahmoud.
Kwa maelezo ya taarifa hiyo lengo la mashindano hayo ni kusherehekea
miaka 40 ya kuzaliwa kwa CCM, kuinua vipaji vya vijana katika mchezo wa
mpira wa miguu sambamba na kuunga mkono kauli ya Dk. Shein ya kutaka
Zanzibar iwe na vuguvugu la michezo kwani wanaamini kuwa hoja hiyo
imelenga utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM.
Vijana hao pia, walitoa salamu zao za dhati kwa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tazania John Pombe Magufuli kwa jitihada zake za kupambana
na biashara haramu ya madawa ya kulevya.
Mshindi wa kwanza wa mashindano hayo atapata kikombe, gari na nishani
ambapo mshindi wa pili atapata milioni tatu na mshindi wa tatu atapata
milioni mbili pamoja na zawadi nyengine zitakazotolewa katika mashindano
hayo.
Mbunge wa Jimbo la Mpendae Salim Turky kwa upande wake akiwa pia, ni
mkereketwa wa michezo hapa nchini aliahidi kununua gari hiyo kwa ajili
ya mshindi wa kwanza wa mashindano hayo ambapo wafanyabiashara wengine
na wakereketwa wa chama hicho waliahidi kuchangia mashindano hayo
zikiwemo fedha taslim.
Miongoni mwa Timu zitakazoshiriki mashindano hayo ni Jimbo la
Mpendae, Jangombe, Kikwajuni, Kwahani, Amani, Shaurimoyo, Chumbuni,
Malindi, Magomeni, Kiembesamaki, Mfenesini, Dimani, Mahonda, Uzini,
Kaskazini A, Kusini, Afisi Kuu ya CCM pamoja na timu ya CCM Family.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
chanzo:zanzibar24.
Comments