Zanzibar kuagiza mchanga nje ya nchi.

hamadiSerikali ya Mapinduzi ya Zanzibar  imesema imekusudia kuagiza mchanga nje ya nchi kutokana na kupungua kwa kiasi kikubwa kwa rasilimali hiyo hapa nchini.

Akizungumza na Waandishi wa Habari, Waziri wa kilimo Maliasili Mifugo na uvuvi Hamad Rashid amesema Zanzibar  haina mchanga utakaokidhi  mahitaji ya ujenzi   kutokana na   kiwango  kikubwa cha rasilimali mchanga kuchimbwa kwa kasi  unguja na pemba.

Hata hivyo amesema ili kupunguza tatizo hilo lazima serikali  kutumia matumizi mbadala  wa mchanga  katika harakati za ujenzi  au mbinu za kutumia mchanga kidogo na kubuni  rasilimali nyengine  badala ya mchanga ili kupunguza tatizo ambalo linaathiri  hapa nchini.

Aidha amesema  hali imekuwa mbaya kutokana na  matumizi mabaya ya ardhi inayosababisha athari kuongezeka  hivyo serikali  inatumia hatua za dharura kudhibiti  uchimbwaji wa mchanga lazima  utaratibu  wa utoaji vibali  ubadilike  kutokana  na upungufu uliopo  ili kudhibiti rasilimali chache ilobaki.

Ametoa wito kwa wananchi kuwacha  kuchimba mchanga  kiholela  na wanaochimba  katika maeneo ya kuvunia kuwachana na serikali itatenga maeneo mbadala yatakayo tumika kwa shughuli hizo na kwa utaratibu maalum.

Utafiti  uliofanywa hivi karibuni kwa Unguja na Pemba imeonesha kuwa   Unguja inachimba hekta 3  kila mwezi na Pemba nusu hekta kila mwezi ambapo kwa mwaka  2016 uchimbaji huo umefikia tani  Million moja laki nane na arobaini na sita elfu.

chanzo;Zanzibar24

Comments